
Na Mwandishi Wetu, Lindi
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amewaambia wananchi wa Lindi kuwa shughuli ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo bado haijaisha, akisema kuna kazi kubwa itafanyika ndani ya miaka mitano ijayo.
Dkt. Samia ameeleza hayo Jumatano Septemba 24,2025 akihutubia maelfu ya wananchi wa Ruangwa katika uwanja wa Madini wilayani humo, mkoani Lindi.
Amesema mambo yaliyofanyika ndani ya miaka mitano wilayani Ruangwa mkoani Lindi katika sekta za afya, elimu, maji, umeme yamesemwa na waliotangulia kuzungumza, lakini maendeleo ni hatua na mwendelezo.
“Pamoja na yote yaliyofanyika bado kuna maeneo ya kipaumbele ambayo bado yanahitajika kufanyiwa kazi.Niwaahidi nitaendelea kufanya kazi katika sekta zote za maendeleo ya jamii ili Ruangwa kuendelea zaidi,”
“Tutakuja kujenga vituo vya afya, zahanati, shule za msingi na sekondari, tutahakikisha miradi yote yam aji inayotekelezwa inakamilika ili kila MwanaRuangwa kupata majisafi na salama,”
Ameongeza kuwa, “Tunakwenda kumaliza kuunganisha umeme katika vitongoji ili utumike kwenye makazi, kulinda usalama wa wilaya na kuzalisha kwa sababu tutaweka kongani ya viwanda. Niwaahidi kazi bado ipo na tunakuja kuifanya,” amesema Dkt Samia.
Katika hatua nyingine,Dkt. Samia amempongeza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika kipindi chote walichoshirikiana Serikali akiwaahidi wananchi wa Ruangwa kuwa kiongozi huyo, atabaki kuwa msaidizi na makini katika Serikali.
“Ahadi yangu kwenu, katika kuuthamini na kuutambua mchango wa ndugu yangu Kassim Majaliwa, ameacha kuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Ruangwa anaendelea kuwa msaadizi na muhimu katika Serikali yetu,”
Mbali na hilo, amewapongeza wananchi wa Ruangwa kwa uzalishaji mzuri wa mazao ya biashara na chakula, akiwaahidi Serikali itaendelea kuwashika mkono kwenye ruzuku za mbolea na pembejeo.
“Kubwa zaidi tutaendelea kutafuta masoko na beI kubwa zaidi hii ndio ahadi yetu kwenu,” amesema.





