
Na Mwandishi Wetu, Ruvuma
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema mpango wa Serikali yake katika miaka mitano ijayo ni kuufanya Mkoa wa Ruvuma kuwa kitovu cha biashara katika ukanda wa kusini.
Dkt Samia ameeleza hayo leo, Jumatatu Septemba 22, 2025 alipozungumza na wananchi wa Songea Mjini katika mkutano wa kampeni za urais mkoani Ruvuma.
“Tunataka kuufungua Mkoa wa Ruvuma na ukanda wa kusini kuwa wa biashara. Kwa maana hiyo Mkoa wa Ruvuma tumekamilisha upanuzi na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Songea kuruhusu ndege kubwa kutua hapa,” amesema.
Sambamba na hilo, ameahidi kujenga mitambo katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, kwa ajili ya kuongeza thamani zao la kahawa ili liuzwe likiwa tayari limeshaongezwa thamani.
Dkt Samia amesema ujenzi wa Bandari ya Mbambabay umefikia asilimia 35, huku Bandari ya Ndumbi ikiwa imekamilika na imeanza kuleta tija katika biashara kati ya Tanzania na Malawi.
Amesema wanafungua shoroba mbalimbali ili Ruvuma iwe kitovu cha biashara na kwamba atakapopewa ridhaa atakamilisha mradi wa Barabara ya Kidato-Ifakara-Malinyi hadi Lumecha inayounganisha Ruvuma na Morogoro.
Mradi mwingine alioutaja ni ujenzi wa SGR itakayounganisha Mtwara hadi Mbambabay yenye urefu wa kilomita 1,000 ili kurahisisha usafiri wa madini yatakayochimbwa katika eneo la Liganga na Mchuchuma.
“Tunafungua mkoa huu na shoroba ya kusini kwa njia zote, anga, barabara, reli na maji ili kuufanya ukanda huu uwe ukanda wa kibiashara,” amesisitiza.


