Dkt. Ndumbaro: Sheria 300 zimebadilishwa kutoka Lugha ya Kingereza kuwa Kiswahili

Na Salha Mohamed

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, amesema tayari sheria 300 kati ya 446 zimebadilishwa kutoka lugha ya kingereza kuwa kiswahili.

Hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Mwanasheria Mkuu wa serikali kukamilisha shughuli ya kutafsiri sheria za Tanzania kwa lugha ya Kiswahili.

Kutokana na hali hiyo, Dkt. Ndumbaro ameipongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa sheria kwa kuendelea kutafsiri sheria hizo lengo likiwa kusaidia wananchi kuweza kuzielewa sheria za nchi.

Hayo yamebainishwa leo alipotembelea maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwàlimu Nyerere vilivyopo Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Amesema ofisi hiyo ni muhimu kwasababu bila ya ofisi hiyo hakuna sheria itakayokwenda bungeni kutungwa.

“Hii ni ofisi muhimu sana bila ofisi hii hakuna sheria inayokwenda bungeni kutungwa, hakuna sheria itakayofanyiwa marekebisho bungeni wala hakuna sheria ndogo itakayotungwa wala kufanyiwa urekebu,” amesema.

Amesema katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga bajeti ili waweze kutafsiri sheria zilizobaki 146 ili kukamilisha sheria zote 446 lengo watanzania waweze kuzielewa kwani hiyo ndio kazi yao kuu.

“Hii ni ofisi muhimu sana kwani ikifa ofisi hii hata mahakama itavurugukiwa kwani itakuwa inatumia sheria ambazo hazipo sahihi, kazi ya ofisi hii muhimu katika mustakabali mzima wa kutunga na kuchakata sheria za nchi,” amesema Dkt. Ndumbaro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *