Na Penny Yohana, Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais Dkt. Philip Mpango, ametoa wito kwa nchi wanachama zisizofungamana na upande wowote.
Alizitaka nchi hizo ziendelea kufanya kazi kwa mshikamano, kutumia fursa, kukuza biashara ya kimataifa na uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kiuchumi pamoja na mbinu bora.
Dkt. Mpango aliyasema hayo jana wakati akihutubia mkutano huo uliolenga kujadili namna ya kukabiliana na athari za Uviko-19 uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Baku, nchini Azerbaijan.
Alisema janga la Uviko-19 limetoa somo la kutotegemea msaada wakati wote hivyo nchi wanachama ziwekeze katika tafiti na maendeleo ili kutatua changamoto za ndani ya nchi katika bioteknolojia, utengenezaji chanjo, vifaa tiba, bidhaa, vitendanishi ili kuokoa maisha ya wananchi.
Alitoa wito kwa nchi wanachama kuimarisha uwezo katika ufuatiliaji ili kutambua kwa wakati na kuzuia magonjwa ya kuambukiza kwa manufaa ya afya ya umma.
Pia alizitaka nchi wanachama kujumuisha ujenzi wa miundombinu, mifumo thabiti ya afya, kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya ili kudhibiti milipuko.
“Ni muhimu kuimarisha lishe bora, ustawi wa kimwili wa wananchi ambao ni muhimu kwa maisha yenye afya na ustahimilivu wa magonjwa.
“Natoa wito wa ushirikiano wa kina baina ya mataifa yanayoendelea, kuimarisha uhusiano na nchi zilizoendelea, zinazoendelea, kuheshimiana kwa maslahi ya ustawi wa pamoja,” alisema.
Dkt. Mpango alisema Tanzania inaendelea kutoa wito wa kukomeshwa vikwazo vya kiuchumi, kibiashara na kifedha vilivyowekwa na mataifa makubwa kwa Jamhuri ya Cuba, Jamhuri ya Zimbabwe.
Akitoa uzoefu wa Tanzania kukabiliana na athari Uviko-19 , alisema serikali ilihamasisha utoaji chanjo, kusambaza chanjo kwa walengwa ambayo ilisaidia kudhibiti janga hilo, kuongeza miundombinu ya kutolea huduma za afy, kuongeza watoa huduma, vifaa tiba na dawa muhimu.
Aliishukuru Jumuiya ya nchi zisizofungamana na upande wowote kwa sauti iliyowezesha kupokea chanjo zinazohitajika wakati wa janga hilo.
Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kutumia mkopo wa masharti nafuu chini ya dirisha la Rapid Credit Facility (RCF) kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ili kuongeza uwezo wa miundombinu katika elimu, afya na maji.
Lengo ni kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza, kutoa msaada kwa sekta zilizoathirika zaidi ikiwemo utalii, viwanda na biashara.