Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, amevitaka vikundi vya maendeleo vilivyonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri kuitumia kwa matumizi sahihi ya kujikwamua kiuchumi.
Aidha, amewataka kukumbuka kuirudisha kwa wakati ili kutoa nafasi kwa vikundi vingine kukopa.
Mgomi ameyasema hayo jana wilayani Ileje, wakati wa hafla ya uzinduzi wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mgomi amevipongeza vikundi vya maendeleo vilivyopata mkopo huo sambamba na kuvihimiza kuwekeza katika shughuli walizojipangia ili kupata faida pamoja na kurudisha marejesho ya mkopo huo.
Mgomi pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali masilahi ya wananchi wa wilaya hiyo kupitia mikopo hiyo inayolenga kuimarisha hali ya kiuchumi ya vikundi vya maendeleo.
Katika hatua nyingine Mgomi amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje, Nuru Kindamba, kwa kusimamia na kuhakikisha utoaji wa mikopo linakwenda vizuri.