Na Mwandishi Wetu, Ddodoma
FAINALI ya Wanawake ya mashindano ya Klabu Bingwa ya mpira wa kikapu nchini “betPawa NBL”, itafanyika kesho Novemba 20, mwaka huu kwa mechi ya DB Lioness dhidi ya Fox Divers kwenye Uwanja wa Chinangali, mkoani hapa.
Fainali hiyo imepangwa kuanza saa 12 jioni, inatarajiwa kuwa na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wa timu zote mbili.
Fox Divaz imefuzu hatua hiyo baada ya ushindi dhidi ya JKT Stars wa vikapu 75-62 wakati DB Lioness imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Vijana Queens kwa 48-44.
Kabla ya mchezo huo wa fainali, kutakuwa na michezo miwili. Mchezo wa kwanza utakuwa wa kumsaka mshindi wa tatu kati ya Viipers Queens dhidi ya Orkeeswa kuanzia sa 10 jioni kwenye Uwanja wa Chinangali A na kufuaTiwa na mchezo wa “Classification” kati ya Viipers Queens dhidi ya Orkeeswa kwenye uwanja wa Chnangali B.
Washindi kwa upande wa wanaume na wanawake watazawadiwa sh. milioni 2.8 kila mmoja wakati washindi wa pili watazawadiwa sh. milioni 1.4.
Fedha hizo zimetolewa na wadhamini wakuu, betPawa ambapo zaidi ya sh. milioni 144 zimetengwa kwa ajili ya kugharimia gharama mbalimbali pamoja na zawadi.
Washindi wa tatu kwa wanawake na wanaume watazawadiwa sh. 700,000 ambapo wachezaji bora wa mashindano (MVP) kwa wanawake na wanaume kila mmoja atazawadiwa sh. 700, 000.
Pia kutakuwa na zawadi ya wafungaji bora, mabeki bora na “best rookie” kwa wanawake na wanaume ambapo watazawadiwa sh. 420, 000 kila mmoja na zawadi ya ‘sportsmanship’ kwa wanawake na wanaume itakuwa sh. 280,000.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF), Mwenze Kabinda, wanatarajia ushindani mkali katika michezo hiyo ya mwisho kwani kila timu imeundwa na wachezaji nyota.
“Si unajua kuwa kila timu inayoshinda, wachezaji 12 na viongozi wanne wanapewa fedha taslimu sh. 140,000 kutoka kwa wadhamini, wakuu, betPawa.
Kwa upande wa Meneja wa Masoko wa Kanda ya Afrika Mashariki wa betPawa, Borah Ndanyungu, amesema wanajisikia fahari kuwa miongoni mwa wadau wa maendeleo ya michezo nchini hasa mpira wa kikapu.
“Kampuni yetu, betPawa imedhamiria kuleta maendeleo chanya ya mchezo na tunaamini tutafikia lengo hilo,” amesema.