Na Is-Haka Omar, Zanzibar
AZMA ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ni kujitegemea kiuchumi kupitia vyanzo vyake vya mapato. Ili kufikia malengo hayo kimekuwa kikihamasisha mwelekeo wa siasa na uchumi.
Mwelekeo huo siyo tu ufuatwe na kusimamiwa na viongozi wa juu, bali katika kila ngazi ya chama hicho kinachoshikilia dola.
Dhamira hiyo ya CCM, inatekelezwa kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ili kukusanya mapato yatakayoiwezesha kujitegemea.
Februari 18, 2023 CCM kwa upande wa Zanzibar kilifungua mradi mkubwa wa kimkakati na kihistoria wa maduka ya kisasa unaojulikana kama ‘Darajani Souk’ katika eneo la darajani mjini hapa.
Akizindua mradi huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, alikisisitiza chama hicho kikongwe nchini kusimamia vizuri mapato yanayotokana na mradi huo, sambamba na kubuni miradi mingine ya maendeleo.
Alisema mradi wa maduka hayo ya Darajani ni sehemu ya jitihada za kutekeleza ilani ya uchaguzi wa CCM, “Tulipokuwa kwenye kampeni za uchaguzi mkuu uliopita tuliwaahidi wafanyabishara wadogo kuwa tutawajengea maeneo mazuri ya kufanyia biashara.
“Tuulinde na kuuendesha vema mradi huu ili kufanikisha dhamira ya chama kubuni miradi mikubwa ya kiuchumi yenye kuingiza fedha nyingi zitakazosaidia kukuza, kuimarisha chama na jumuiya zake,” alisema Dkt. Mwinyi.
Dkt. Mwinyi alisema mbali na mradi huo pia Serikali inaendelea kujenga masoko katika wilaya zote za Unguja na Pemba ikiwemo masoko makubwa kama Chuini, Jumbi, Mwanakwerekwe na Mombasa.
“Wananchi na wafanyabiashara mliohudhuria katika hafla hii nawajulisha kuwa CCM itaendelea kubuni miradi mikubwa ya kiuchumi na uwekezaji ili kukijenga chama kwa nguvu za kiuchumi.
Malengo haya tunayafanyia kazi kwa vitendo ili kila mwananchi apate fursa ya kufanya biashara za kujiingizia kipato na kujikwamua kiuchumi,” alisema Dkt. Mwinyi.
Katika hatua nyengine Rais Mwinyi aliwanasihi wafanyabiashara watakaobahatika kupata milango, kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
Pia aliwataka viongozi wa chama kutumia busara ya ugawaji wa maduka hayo, “Kipaumbele cha kwanza wapewe wale wote waliopisha mradi huu, waliolazimika kusitisha shughuli zao za biashara na kuacha ujenzi uendelee.
Alisema Serikali imeruhusu biashara katika eneo hilo kufanyika saa 24, “Niwahakikishie wafanyabiashara mtakaokuwa mkifanya shughuli zenu hapa ulinzi wenu na mali zenu utakuwa wa uhakika, ila niwashihi kuendelea kuitunza haiba ya mji kwa kuweka mazingira safi na salama, fanye ukarabati mnapoona sehemu imeharibika ili maduka yadumu muda mrefu na kuleta tija iliyokusudiwa.
“Sote tunaimani njema ya kuutunza Mji Mkongwe, ni urithi wetu sisi na vizazi vijavyo, hatuwezi kuruhusu uharibike na tumetengeneza maduka haya eneo la Darajani ili liwe na taswira yenye hadhi ya mji wa biashara,” alisema Dk Mwinyi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Masoud Ali Mohammed alisema Serikali inatekeleza ahadi zake kwa vitendo, huku akiwasihi wananchi kuacha chuki, kebehi na lawama.
“Hizi hazijenge nchi nawaomba mshirikiane kwa kupeana moyo ili kuendeleza uchumi na biashara.”
Awali akisoma risara ya mradi huo mbele ya Rais Mwinyi, Katibu wa Kamati Maalumu NEC, Idara ya Uchumi na Fedha, Afadhali Taibu Afadhali, alisema mradi wa maduka hayo unamilikiwa na CCM.
Alisema mradi huo ni utekelezaji wa sera ya chama hicho, toleo la 2021 inayokitaka kutekeleza miradi na uwekezaji na kuelekeza kazi zote za chama kujikita kwenye kujenga uchumi na uwekezaji.
Alisema mradi huo una jumla ya maduka 445 yenye miundombinu rafiki ya kufanyia biashara, hasa kwa wafanyabishara na wajasiriamali wadogowadogo.
Alifafanua eneo hilo awali lilikuwa na maduka 58 yenye wafanyabishara 168, ambao walikubali kuondoka kwa hiari ili kupisha ujenzi huo kwa makubaliano ukikamilika watapewa kipaumbele kwa kupewa maduka ili waendelee kufanya biashara.
“Nawasishi wawekezaji mje kuwekeza katika maeneo na miradi mbalimbali ya CCM, iliyopo na inayoenelea kubuniwa na kutekelezwa kila mara,” alisema Afadhali.
Naye Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis alisema mradi huo ni wa kihistoria kwani umeendana na dhamira ya CCM ya kujiimarisha kiuchumi katika kufikia maendeleo endelevu.
Mbeto alisema sura ya pili ukurasa wa 9 hadi 10 katika Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 imeelekeza kufanyika kwa mapinduzi ya kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji wenye tija.
Katibu huyo alitumia fursa hiyo kumueleza Rais Mwinyi kuwa CCM inapata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa serikali hatua inayoongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Mafanikio haya yanatokana na juhudi za Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wake Dk Mwinyi ambao kwa pamoja wamekuwa wakifanya kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo endelevu kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo,” alisema Mbeto.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Idrisa Kitwana alisema Serikali inaendeleza miradi mingine ya kisasa itakayotoa faida kwa wananchi ikiwamo miradi ya maegesho ya magari ya kisasa kwenye eneo la mji wa Darajani.
Kwa upande wa mwekezaji wa mradi huo kutoka kampuni ya Africab, Yussuf Azzi alipongeza juhudi za Serikali ya awamu ya nane kwenda na kasi ya kuimarisha miundombinu rafiki ya kibiashara itakayochangia kutoa ajira kwa wananchi.
Alisema mradi huo umegharimu Sh7.5 bilioni hadi unakamilika.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa mjini wa Zanzibar walisema kuwa mradi huo wa maduka utapunguza uwepo wa msongamano wa watu katika eneo hilo la Darajani.
Ibrahim Faki Ibrahim, Mkazi wa Kiponda, aliipongeza CCM kwa kujenga maduka hayo ya kisasa yanayoendana na hadhi ya jiji la Zanzibar.
Naye mkaazi wa shehia ya Malindi Zainab Khamis Juma, alisema uchumi wa Zanzibar unategemea utalii, hivyo ni lazima maeneo ya mjini yawe na haiba na mwonekano wa kisasa, kwani ndio mlango mkuu wa kupitia wageni wanapoingia nchini.
“Binafsi naunga mkono dhamira ya Rais Mwinyi ya kujenga na kufanya matengenezo makubwa ya miundombinu hapa Darajani, ili liwe eneo la kisasa linaoendana na miji maarufu ya kibiashara duniani,” alisema Zainab Khamis Juma, mkazi wa Shehia ya Malindi.
“Kutokana na wageni wengi wanaoingia hapa nchini bila shaka ipo haja ya kuwa na miundombinu mingi ya aina hii,” alisema Mohammed Said Faki, mkazi wa Mwembeladu.