
Na Mwandishi Wetu, Arusha
MGOMBEA urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt Samia Suluhu Hassan amesema hatua ya Serikali yake kuboresha huduma za afya nchini, imemshangaza Dk Steve Meyer aliyewafadhili matibabu na masomo majeruhi wa ajali ya Shule ya Lucky Vicent.
Ajali hiyo ya basi la Shule ya Msingi Lucky Vincent ilitokea Mei 6, 2017 katika eneo la Rothia wilayani Karatu mkaoni Arusha na kusababisha vifo vya watoto 33, walimu wawili na dereva mmoja.
Baada ya ajali hiyo, Dkt. Meyer amewafadhili majeruhi kadhaa kwenda nchini Marekani kwa matibabu na masomo ya elimu ya msingi hadi elimu ya juu.
Dkt. Samia ametoa kauli hiyo leo, Alhamsi Oktoba 2, 2025 alipozungumza na wananchi wa Arusha Mjini katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Kaluta, katika mwendelezo wa kampeni zake za urais.
Amesema hivi karibuni (Novemba 2, 2024) alikutana na Dk Meyer aliyewachukua wanafunzi wanne kuwapeleka Marekani na walipokutana alifanya ziara katika hospitali mbalimbali nchini.
“Alipokuja alifanya ziara kwenye hospitali zetu. Alifanya ziara kwenye hospitali ambayo mwanzo wale watoto walipelekwa ilishindikana matibabu kabisa.
“Baada ya kuona hospitali ilivyotengenezwa na vifaa vilivyomo, Dk Meyer alikuja kuniona akasema umefanya miujiza gani. Akasema ile ajali ingetokea sasa hivi watoto wale tungewatibu hapa hapa bila kuwasafirisha,” amesema.
Dkt. Samia amesema hospitali kwa sasa vimewekwa vipimo mbalimbali na kwamba kuna hospitali zinazotoa matibabu nchini bila kulazimika kusafiri nje ya nchi.


