Na Victor Masangu, Kibaha
UJUMBE wa Chama cha Kikomunisti cha nchini China (CPC) kimesema kinakumbuka mchango wa Tanzania kurudishiwa kiti chake katika Umoja wa Mataifa (UN) Mwaka 1973.
Komredi Mao Dingzhi, Naibu Waziri wa Idara ya Oganaizesheni ya Kamati Kuu ya chama cha (CPC), Komredi Mao Dinghi, akizungumza wakati wa ziara yake wilayani Kibaha, mkoani Pwani na wana-CCM, amesema nchi za Afrika ikiwamo Tanzania zilikuwa kinara wa harakati za kiti cha China kinarejeshwa UN.
Komredi Mao amesema mambo mengi ya maendeleo yanayoyafanya nchini na Taifa la China ni kukumbuka na kulipa fadhila za jitihada zilizofanywa na CCM na nchi ya Tanzania chini ya uongozi imara wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kuhakikisha kiti cha Taifa la China UN kinarejeshwa.
Amesema CPC na Taifa la China wanakumbuka na kuthamini mchango huo wa Tanzania kupitia Balozi wake wakati huo katika Umoja wa Mataifa, Dkt. Salim Ahmed Salim.
Akizungumzia muundo wa chama cha hicho, unaanzia ngazi ya chini kwenda ngazi ya juu kama kilivyo CCM ambapo pia CPC hutilia mkazo sana ngazi ya chini ya Uongozi kuwa na nguvu zaidi ya ngazi za juu.
Akiwa kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere Kibaha mkoani Pwani Komredi Mao, ametembelea na kukagua majengo ambayo ujenzi wake unanufaisha viongozi vijana wa nchi sita za kusini mwa Afrika ambazo zilishiriki harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.
Aidha, amemkabidhi Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julias Nyerere Prof. Marceline Chijoriga vitabu vinane vya masuala ya uongozi ambavyo vinaelezea namna Taifa la China lilivyopiga hatua za maendeleo ili na viongozi wa nchi hizo sita zinazofika kusoma shuleni hapo waweze kujifunza ili nao wapige hatua za maendeleo.
Naye Prof. Chijoriga ameomba Uongozi huo wa Chama Cha CPC, kuandaa mafunzo maalumu kwa viongozi wa CCM na wa nchi sita zilizoshiriki harakati za ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.