Na Sarah Moses, Dodoma.
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inatarajia kuanza kufanya tafiti inayohusu changamoto ya ufaulu katika somo la Hisabati kutokana na kuonekana kwa matokeo mabaya ya kidato cha nne na darasa la saba.
Utekelezaji wake pia unahusisha watafiti kutoka vyuo mbalimbali hapa nchini na itafanyika ndani ya miaka miwili ambapo kwa sasa ipo katika hatua ya kusaini mikataba
Akizungumza Jijini Dodoma leo Agosti 25,2023 Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo Dkt.Amos Nungu amesema kuwa serikali ilifadhili miradi ya utafiti kupitia COSTECH,ambapo baadhi ya miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji .
Amesema kuwa somo la hisabati bado linaonekana ni changamoto kwani matokeo yake yamekuwa mabaya Kwa kidato cha nne na Darasa la nne hivyo kwa kubaini chanzo cha tatizo hilo wao kama Tume wameidhinisha miradi miwili ambayo kila mmoja thamani yake ni milioni 120.
“Kutokana na kuwepo kwa changamoto ya matokeo mabaya ya somo la hisabati katika matokeo ya darasa la Saba na kidato cha nne COSTECH imefadhili ili kuona tatizo ni nini mpaka wanafunzi wanafeli somo hilo”amesema.
Kila matokeo yanapotoka Darasa la Saba na Kidato cha Nne, Somo la Hisabati limeonekana kuwa changamoto,Serikali kupitia COSTECH imeidhinisha miradi miwili kwa thamani ya TZS 120M kila mradi. .
Aidha amebainisha kuwa CHOSTECH inafanya ufuatiliaji wa miradi inayohusu kuboresha maabara za utafiti kwa ukarabati na ununuzi wa vifaa vya kisasa ikiwemo, Maabara ya Utafiti wa Baharini katika Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar mradi ambao tayari ulishakamilika.
Vilevile Mkurugenzi huyo amesema Serikali kupitia COSTECH imeidhinisha jumla ya miradi saba ya thamani ya shilingi mil. 150 kila mradi.
“Miradi hii itafanyika ndani ya miaka miwili na inahusisha watafiti na wabunifu kutoka sekta zote” amesema
Hata hivyo COSTECH inaendelea kuimarisha mfumo wa ubunifu nchini kwa kuanzisha au kutoa usaidizi kwa vituo mbalimbali vya ubunifu (intemediaries) ili kuwafikia na kuwahuduma wabunifu kiurahisi.
Mwisho.