COSOTA yafanikiwa kusuluhisha migogoro 118

Na Sarah Moses, Dodoma.

IMEELEZWA kuwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya Sita Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imefanikiwa kupokea  jumla ya migogoro 136 na kusuluhisha migogoro 118. 

Hayo ameyasema Machi 21,2025 jijini Dodoma Afisa Mtendaji Mkuu na Msimamizi wa Hakimiliki Doreen Sinare wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mikakati ya COSOTA katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.

Amesema migogoro 10 kati ya hiyo haikumalizika na ilifunguliwa kesi mahakamani na migogoro 8 inaendelea COSOTA lakini pia  sambamba na migogoro hii, COSOTA imehusika na kesi za hakimiliki 10.

Pia amesema katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita Muziki wa singeli ambao ni wa kipekee kutoka Tanzania umekuwa kwa kasi na kupendwa naidi nchini na kuvuka mipaka ya nchi. 

“Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano alieleza namna alishuhudia wazungu wakifurahia Muziki huo,” amesema 

Katika kipindi hiki, COSOTA imetoa elimu kwa Wasanii, watayarishaji, wafanyabiasha na wadau wa Singeli kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Uswazi Got Talent na Kandoro Baba Entertainment chini ya Meneja Kandoro na Kituo cha cha redio na televisheni kupitia Efm kikiendeshwa na Samio Love kuwaeleza umuhimu wa usajili wa kazi zao na faida za kusajili ambapo takribani wasanii 20 wa Muziki wa Singeli wamesajili kazi zao COSOTA. 

Lakini pia wamenufaika na mgao wa mirabaha kwa mwaka 2022 na mwaka 2023 na nimategemeo yetu kuwa watanufaika Zaidi kutokana na kupendwa na kushiriki katika biashara ya muziki wa singeli ndani nan je ya nchi.

“Ni matarajio ya COSOTA kuwa mafanikio haya ni chachu ya ukuaji wa biashara ya tasnia ya hakimiliki sasa na miaka ijayo ambapo yataongeza kipato kwa wasanii, waandishi na wabunifu wenye hakimiliki na kutengeneza ajira zaidi sambamba na kuongeza pato la taifa. Kazi iendelee” amesema Doreen.

Hata hivyo katika hatua nyingine Mkurugenzi huyo amesema usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria ya hakimiliki na hakishiriki umeongezeka kwa asilimia 70 Ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kuanzia mwaka 2021 mpaka Februari 2025, COSOTA, imesajili kazi za Sanaa na uandishi 11,519 na Wabunifu 3,436.

“Idadi hii ya wabunifu pamoja na kazi zao imetokana na zoezi la utoaji wa elimu na mafunzo mbalimbali ya hakimiliki na usajili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina lakini pia kushiriki matukio mbalimbali ya wadau ambapo COSOTA ilipata fursa ya kuelimisha wadau kuhusiana na hakimiliki na uhamasishaji wa usajili wa kazi za hakimiliki” amesema.

Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *