Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo ameeleza kuwa, kwa sasa hakuna Chama chochote cha siasa au mtu yeyote aliye na uhitaji mkubwa wa Katiba iliyo bora na yenye manufaa kwa Watanzania kuliko CCM.
Chongolo ametoa kauli hiyo leo alipowasili wilayani Mufindi mkoani Iringa ikiwa ni Siku ya kwanza ya Ziara yake ya Siku 7 yenye lengo la Kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020/2025.
Akizungumza na Wananchi pamoja na Wana CCM mara baada ya Kuwasili katika halmashauri ya wilaya ya Mufindi Chongolo amewatoa wasiwasi Wananchi katika eneo hilo akisema kuwa Kazi ya Ujenzi wa nchi sio nyepesi inahitaji watu wote kuwa Sawa.
“Nimesikia sikia huko watu wanasema sema kuhusu katiba mpya, labda niwaambie tu kwamba CCM tunahitaji katiba iliyobora kuliko mtu yoyote yule, ndio Maana Chama cha Mapinduzi kimempa ridhaa na dhamana mwenyekiti wake na Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kuanzisha mchakato wa mapitio kuhusiana na suala la Katiba mpya” amesema Chongolo.
Katibu Mkuu Chongolo ameambatana na Wajumbe wawili wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Katibu wa NEC Oganaizesheni Ndugu Issa Haji Ussi (Gavu) na Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndugu Sophia Mjema.