Chongolo anavyochochea kasi mbio za Samia kuwaletea wananchi maendeleo

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amefanya ziara ya siku tisa katika mkoa wa Morogoro na kuhitimisha kwa kufunga kero zilizolalamikiwa na wananchi wa mkoa huo.

Chongolo amekutana na kero katika maeneo alikopita ya vijiji, kata na wilaya za mkoa huo katika sekta za maji, umeme, barabara, afya, elimu, ardhi na kilimo.

Katika ziara hiyo, Chongolo ameongozana na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema na Katibu wa NEC na Oganaizesheni, Issa Gavu, kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, uhai wa chama, kusikili na kutatua kero za wananchi.

Alivyotatua kero

Akiwa katika maeneo mbalimbali, Chongolo akatumia utaratibu wa kusikiliza kero za wanachama na wananchi aliokutana nao, kwa kuwa CCM ndicho chama chenye dhamana ya kuongoza serikali.

Akatumia utaratibu wa kusimamisha watendaji wa serikali wakiwamo wa ngazi ya vijiji, kata, wilaya, mkoa na wizara.

Kila alikopita aliwatumia watendaji wa sekta zote waliopewa dhamana katika mkoa huo kujibu kero na maswali waliyouliza wananchi kwa lengo za kuzitatua na kuzitafutia ufumbuzi.

“CCM ndicho chama chenye dhamana ya kuongoza nchini, ndiye mmiliki wa duka, tuna haki ya kuhoji, kuagiza na kuchukua hatua, kwenye mambo ambayo hayaendi sawa,” akasema Chongolo.

Kituo cha Afya kutotumika

Akiwa Kijiji cha Mikese, Chongolo akakuta Kituo cha Afya cha Mikese, ambacho baadhi ya majengo yamekaa zaidi ya miaka mitatu bila kutumika kwa kukosa vifaa vya matibabu.

Chongolo alichukizwa na tukio hilo lililofanywa na Halmashauri ya Morogoro Vijijini, ambayo imeshindwa kutumia Sh. 50 ya fedha zake za ndani, kununua vifaa vichache ili jengo la wazazi lianze kutoa huduma, wakati wakisubiri vifaa vinavyopelekwa na serikali.

Akashangazwa na halmashauri hiyo kuwa na bakaa ya Sh. bilioni 2.5 iliyobaki kwenye bajeti ya mwaka wa fedha uliopita.

“Hatuwezi kwenda namna hii, nitaenda kuzungumza na Waziri wa TAMISEMI aje mwenyewe hapa ndani ya siku 14, aone fedha zilizowekwa hapa kwa ajili ya kujenga majengo haya lakini hayatumiki, haiwezekani.

“Hata tukiwaleta watumishi wa afya waliopangwa hapa nadhani wanatushangaa maana hawana kazi ya kufanya, madaktari nao hawana kazi wanatamani vifaa vingekuwepo wafanye kazi,” akasema Chongolo na kuongeza kuwa;

“Na sisi tukija hapa tunasema kidumu chama cha mapinduzi, kitadumu kama mambo yatanyooka hivi hatuwezi kudumu kama wenyewe tunajihujumu, haiwezekani hata kidogo. Nimechaguliwa kuwa, Katibu Mkuu wa chama nikaona mambo ya hovyo nikapiga makofi hapa, nitakuwa simtendei haki aliyenipa dhamana hii Mwenyekiti wangu wa chama ambaye pia ni Rais wa Tanzania.”

Kusuasua ujenzi barabara

Chongolo akiwa mji wa Ifakara wilaya ya Kilombero, anakuta ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara yenye urefu wa Kilomita 66.9 kwa kiwango cha lami ikiwa haijakamilika.

Akamuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania mkoa  (TANROADS) Mhandisi Lazack Kyamba, kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza mradi huo kamilishe mradi huo kufika Octoba 15, mwaka huu.

Chongolo akasema haiwezekani ujenzi huo uchelewe wakati fedha za utekelezaji wake tayari zilishatengwa na kuonya wasimamizi watakao kaidi maelekezo hayo ya Chama.

“Dhamira ya Serikali ya CCM ni kuwaletea maendeleo Watanzania kwa kuwaondolea changamoto ikiwamo za miundombinu ya barabara ili wafike wanakotaka kufika kwa wakati,” akasema Chongolo.

Fidia mashamba

Akiwa katika Kijiji cha Melela, wilayani Mvomero, akakutana na kero ya wananchi kutolipwa fidia ya mashamba 2,005 yaliyovamiwa na wanyama wakimo Tembo.

Katika uvamizi huo, anaelezwa kuwa, wananchi 30 watarafa saba za kijiji hicho, walipoteza maisha.

“Changamoto haijibiwi kwa maneno mengi, kama Tembo walivamia maeneo ya watu, Waziri ya Maliasi na Utali, (Dk. Pindi Chana) au watendaji wa wizara na kuna mamlaka zake zilizopewa majukumu, ndani ya siku saba wafike hapa kuzungumza na wananchi,” akasema Chongolo na kuongeza kuwa,

“Tembo wamekula mazao, watu walipwe fidia, kinachotakiwa fedha ilipwe kwa walioharibiwa mashamba yao, waje hapa wakae na nyie mpate haki yenu.”

Vijiji visivyo na umeme

Akiwa nyumbani kwa Katibu wa Shina Namba 10 la chama hicho, Zainabu Ajili Ally wa Kijiji cha Dumila Juu, katika Kata ya Dumila, Wilaya ya Kilosa, akakutana wananchi wa vijiji 68 wakilalamikia kukosa huduma ya umeme.

Aidha, wanalalamikia kuunganishiwa kwa Sh. 310,000 badala ya Sh. 27,000 iliyopangwa ma serikali kwa maeneo ya vijijini.

Akawaahidi wananchi hao kuwa, Aprili mwaka huu, ataongozana na Waziri Nishati, January Makamba kuwasha umeme katika vijiji vyote vya wilaya hiyo ambavyo havina huduma hili ilihali serikali imetoa fedha za kutekeleza mradi wa umeme vijijini.

Chongolo akamtaka Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO), Fadhili Chilombe, kujibu kero hiyo, ambaye anasema kuwapo kwa gharama hizo kulitokana na kutokuwapo na mawasiliano sahihi huko nyuma.

“Kulikuwa kuna tatizo la mawasiliano ndio sababu ya kutozwa kiasi hicho, lakini kuanzia sasa watatozwa Sh. 27,000 badala ya 310,000.”

Wakulima kupunjwa utamu wa miwa

Akiwa wilayani Kilombero, Chongolo akapokea kero ya wakulima wa miwa kulalamika kupunjwa malipo ya utamu wa miwa na Kiwanda cha Kuzalisha wa Sukari cha Kilombero.

Katibu CCM Tawi la Sanje- Kidatu, Timotheo Kihanji, akawasilisha kero hiyo, kwa niaba ya wakulima hao ambao wanadai kupewa malipo pungufu kwa madai miwa haina utamu unaokubalika na kiwanda hicho.

Akijibu kero hiyo, Chongolo akamwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Fatma Mwasa, kukaa na Vyama Vya Ushirika wa Kilimo na Biashara (AMCOS), kuteua mkulima mmoja katika kila chama, kwenda kufundishwa namna wanavyopima utamu wa miwa kiwandani.

Akasema wakifundishwa na kufahamu namna kiwango cha utamu wa miwa unavyopimwa, watatoa elimu kwa wakulima wenzao na kupunguza malalamiko ya kero hiyo.

Wenyeviti wa vijiji chanzo migogoro

Chongolo akiwa nyumbani kwa mjumbe wa shina namba tano katika Kijiji cha Itete, wilayani Malinyi, akapokea kilio cha migogoro ya ardhi.

Chongolo, akawaagiza wakuu wa wilaya, kuwachukulia hatua za kisheria ikiwamo kuwaweka ndani, watendaji na wenyeviti wa vijiji ambao wamekuwa chanjo cha migogoro ya ardhi maeneo mbalimbali nchini.

Akasema migogoro mingi ya wakulima na wafugaji inasababishwa na wafugaji kutoheshimu ardhi ya wakulima na kunakosababishwa watendaji na wenyeviti wa vijiji wasiyo waadilifu.

Akasema wafugaji wakipitisha mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima, lazima kuna kiongozi aliyewasaliti wananchi hao na kuruhusu wapite.

“Wakuu wa wilaya simamieni sheria, chukueni hatua madhubuti bila kumwonea mtu, ukibaini kuna mtendaji aliyeruhusu mifugo ikaingia kijijini, kamata sweka ndani, itaweka nidhamu na kudhibiti kukithiri kwa matukio haya ambayo imekuwa kero kubwa nchini,” akasema Chongolo.

Awaweka kitimoto mawaziri

Licha ya majibu waliyotoa kwa wanachi wakiwa katika vitongoji, vijiji na maeneo mbalimbali ya mkoa huo, Chongolo akaendelea kusaka suluhu ya kudumu kutoka ngazi za juu za maamuzi.

Akihitimisha ziara yake mkoani Morogoro, akawaita mawaziri ambao wizara zao zinakero mbalimbali alizokutana nazo.

TAMISEMI 

Mawaziri waliotakiwa kujibu kero hizo ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali (TAMISEMI), David Silinde, ambaye anajibu hoja ya mgawanyo wa walimu kwa usawa katika shule zote za serikali nchini, baada ya Chongolo kulalamikiwa kuwapo kwa upungufu wa walimu vijijini.

Silinde akasema baada ya agizo la Chongolo, tayari wameshatoa barua 545 za uhamisho kwa walimu wa mkoa huo na kutenga Sh. milioni 607 kwa ajili ya kazi hiyo.

“Tangu umetoa agizo la uhamisho, ndani ya siku saba tayari tumeanza kuchukua hatua madhabuti za kuwahamishia walimu katika shule ambazo hakuna walimu wa kutosha ikiwa ni awamu ya kwanza,” akasema Silinde.

Kuhusu Shule ya Msingi Ngerengere, ambayo ilikuwa haijakamilika, akasema wamepokea maelekezo na tayari wametenga Sh. milioni 100 kwa ajili ya kukamilisha ili wanafunzi waanze kusoma.

Alisema kuhusu vifaa vya kutoa matibabu katika Zahanati na Vituo vya Afya mkoani humo, anasema serikali imetenga Sh. bilioni 95.7 na tayari vifaa vimeshaagizwa kwa ajili ya kufungwa na kutoa huduma ya matibabu.

“Kuhusu miradi ya barabara na mingine ya kimkakati ambayo imeshindwa kukamilika kwa wakakati, Waziri wa TAMISEMI, Angela Kairuki, ataanza ziara wiki ijayo katika mkoa wa huu kwa ajili ya kuanza utekelezaji,” akasisitiza.

Akasema barabara ambazo zinaunganisha maeneo ambayo ujenzi wake haujaanza hadi mwezi wa nne utaanza kwa sababu serikali imeshatenga fedha za utekelezaji.

Maji

Chongolo akamtaka Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi, kujibu hoja ya tatizo la kukosekana maji katika baadhi ya maeneo ya mkoa huo ambayo yalilalamikiwa na wananchi katika ziara yake.

Maryprisca akasema, Wizara hiyo inafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wanawake wanapata huduma ya maji nchini ili kuokoa ndoa zao zilizopata shida kutokana na foleni ya kutafuta maji.

Akasema umbali wa kupata huduma ya mbali hautakuwa zaidi ya mita 400 katika maeneo yote nchini.

Akasema kuna Sh. bilioni 72 kwa ajili ya kutatua tatizo la maji vijijini na Manispaa ya Morogoro imetengewa Sh. milioni 165.

“Tumepokea maagizo yote na tutahakikisha tunatekeleza maagizo yote ndani ya muda,” akasema Maryprisca.

Sekta ya ardhi

Katika sekta ya ardhi, Chongolo, akamtaka Naibu wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete, kujibu hoja za malalamiko ya migogoro ya ardhi kukithiri katika mkoa huo.

Ridhiwani akasema kati ya mashamba 77 waliyokagua ambayo hayaendezwi 11 yamefutwa na hekta 2,025 zimegaiwa kwa wananchi.

Akasema katika mkoa huo maeneo yenye migogoro ya ardhi ni wilaya za Kilosa, Mvomero na Kilombero na kwamba wanafanyia kazi kero hiyo kwa kupima maeneo yote nchini yenye migogoro.

Sekta ya mifugo

Katika sekta ya mifugo, Chongolo akamtaka Naibu Waziri wa Mifugo, Abdullah Ulega, kueleza wananchi wa mkoa huo ni kwa namna gani wizara hiyo itamaliza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo inasababishwa na kuhama kwa mifugo.

Ulega akasema suala la mifugo wametenga hekta 500 kwa ajili ya wafugaji wilayani Mvomero.

Akasema wamejenga majosho na kutengeza mabwawa na kuchimba visima kwa ajili ya kutumiwa na mifugo ili kupunguza migogoro hiyo.

Aidha, akasema wanashirikiana na benki kutoa mikopo ya bei nafuu kwa ajili ya wafugaji kufunga kisasa na kumaliza kero ya mufugo kuhama kutafuta malisho.

Wizara ya Kilimo

Chongolo akamtaka Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, kujibu hoja za wakulima kuwa na viwanda vya kuchakata mazao na kuwapo kwa soko la uhakika.

Bashe akasema, serikali inajenga viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali ili kutoa ajira kwa vijana pamoja na kufungua mipaka ili wakulima kuuza chakula nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *