Chongolo ajiuzulu Ukatibu Mkuu CCM

  • Rais Dkt. Samia aridhia, CCM yateua wagombea Mikoa, Wilaya

Na Eckland Mwaffisi, Dar es Salaam

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, ameandika barua ya kujiuzulu katika nafasi hiyo ili kuwajibika kwa maslahi ya chama.

Hivi karibuni, Chongolo alitikisa mitandao ya kijamii kupitia barua iliyokuwa ikisambaa akiomba kujiuzulu.

Barua hiyo ya Novemba 7, 2023 ambayo haijathibitika, ilionyesha kuandikwa, kusainiwa na Chongolo kwenda kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan (Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.

Kwa mujibu wa barua hiyo, Chongolo alimshukuru Rais Dkt. Samia na chama hicho kwa kumuamini, kumlea na kumvumilia wakati wote wa uongozi wake.

Barua ilieleza kuwa; “Mwenyekiti, utakumbuka Aprili 30,2021 Niliteuliwa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kuwa Katibu Mkuu wa CCM.

“Uteuzi wangu ulitokana na mapendekezo yako, upendo na uongozo wako wenye mapenzi mema kwangu, kwa chama pamoja na Taifa.

“Mh. Mwenyekiti, siku chache zilizopita nimechafuliwa kupitia mitandao ya kijamii, hali hiyo imenikumbusha wajibu wa kiongozi kuwajibika kwa maslahi ya chama wakati wote unapotuhumiwa au kuhisiwa kufanya jambo lolote kinyume na kanuni, taratibu, miiko, tamaduni za chama chetu. Mh. Mwenyekiti, naomba uridhie ombi langu kwako la kujiuzulu.

“Natambua kuwa uimara wa CCM unatokana na uongozi wako imara uoanlenga kukuza na kustawisha hali ya maisha ya wananchi kijamii na kiuchumi.

“Mh. Mwenyekiti, sipo tayari kuona Chama Cha Mapinduzi kinachafuka kwa kuhusisha au kunasabisha nafasi yangu ya Katibu Mkuu au uvumi wa matendo, tabia au mienendo ninayochafuliwa nayo.

“Mh. Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa, naomba uridhie ombi langu. Mwisho, japokuwa si kwa umuhimu, nakuombea kwa Mwenyezi Mungu akuepushe, akulinde dhidi ya hila, husda na watu wote wenye nia ovu dhidi yako, chama, serikali, Taifa kwa ujumla, nakuahidi kuendelea kuwa mwana CCM mtiifu wakati wote,” ilieleza barua hiyo.

Taarifa zinasema, barua iliyoandika na Chongolo ya kuomba kujiuzulu nafasi hiyo ni miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa jana katika kikao cha Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam.

Taarifa ya Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari, alisema CCM kimefanya kikao cha kawaida cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, jijini Dar es Salaam.

Kiko hicho kimefanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dkt. Samia. Pamoja na mambo mengine, kikao kilijadili hali ya kisiasa ndani na nje ya chama.

Pia kikao hicho kimefanya uteuzi wa mwisho wa wagombea wa nafasi za uongozi ndani ya chama kwa ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kifo na uteuzi wa nafasi nyingine.

Nafasi ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, wanachama waliojitokeza walikuwa 89, Walioteuliwa ni Dkt. Daniel Mirisho Pallangyo, Loy Thomas Sabaya, Solomoni Olesendeka Kivuyo na Edna Israel Kivuyo.

Mkoa wa Mbeya, wanachama waliojitokeza 48 na walioteuliwa ni Felix Jackson lyaniva, Patrick Adkin Mwalunenge na Fatuma Ismail Kasenga.

Mkoa wa Mwanza, wanachama waliojitokeza 109, walioteuliwa ni Michael Lushinge Masanya (Smart), Sabana Lushu Salinja, Dkt. Anjelina William Samike, Elizabeth Watson Nyingi na David Mayala Mulongo.

Nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya ya Mpanda, wanachama waliojitokeza 36, walioteuliwa ni Hamis Chande Soud, Joseph Aniseth Lwamba, Josephina Yusuph Baraga,  Emmanueli David Manamba.

Wilaya ya Kusini Unguja, wanachama waliojitokeza 15, walioteuliwa ni Maryam Suleiman Haji, Ali Timamu Haji, Mohammed Haji Hassan.

Makonda alisema, kuhusu Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Mwenyekiti wa CCM na Dkt. Samia aliijulisha Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa kupokea barua ya kujiuzulu kwake na ameridhia ombi hilo.

Kikao hicho kimepongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt. Samia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

Chongolo amedumu katika nafasi hiyo kwa siku 942 baada ya kuchaguliwa na Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM Aprili 30, 2021 akirithi mikoba ya Dkt. Bashiru Ally ambaye ni Mbunge wa kuteuliwa.

Dkt. Ally alidumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka miwili na miezi minane baada ya kupendekezwa na Hayati Dkt. Magufuli Mei 29,2018 na kuthibitishwa na w ajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.

Nyota ya Chongolo kupanda kisiasa ilianza kuonekana Juni 27,2016 wakati Rais wa Awamu ya Tano, Hayati Dkt. John Magufuli alipoteua Wakuu wa Wilaya 100, kuwafukuza kazi Wakuu wa mikoa wawili.

Waliofukuzwa kazi ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anna Kilango na Magesa Mulongo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara.

Katika uteuzi huo, Chongolo aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido. Julai 28,2018, Chongolo alihamishwa kutoka Wilaya ya Longido kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, Chongolo alikuwa Ofisa wa CCM kwenye Idara ya Uenezi, Makao Makuu wakati huo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi akiwa Nape Nnauye.

Pia Chongolo amewahi kuwa Mhariri wa Redio Uhuru inayomilikiwa na CCM.

Kwa nyakati tofauti, Chongolo amewahi kuwa Katibu wa Bodi ya Shirika la Magazeti ya Chama (Uhuru na Mzalendo).

Chongolo ameondoka katika nafasi hiyo akiwa Katibu Mkuu wa 10 tangu kilipoanzishwa Februari 5, 1977.

MWISHO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *