China yavutiwa na uongozi wa Samia

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

CHAMA cha Kikomunisti cha China (CPC), kimempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya amani, uhuru wa kutoa maoni, uzalendo, kuheshimu utu wa wananchi wake.

Mkurugenzi Mkuu wa Bureau I, Idara ya Oganaizesheni ya Kamati Kuu ya CPC, Mao Dingzhi aliyasema hayo dare s Salaam jana.

Dingzhi na uongozi wa juu wa CPC ulikutana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ambapo ujumbe huo uliongozwa na Dingzhi akiwa na Balozi wa China nchini, Chen Mingjian

Aliahidi kuendeleza ushirikiano uliopo katika nyanja za uchumi wa kidijitali, kijamii, utamaduni na elimu.

Alisema CPC na Chama Cha Mapinduzi (CCM) vimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu enzi ya waasisi wa vyama hivyo.

Waasisi hao ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung akiongeza, ushirikiano huo unaendelezwa na vyama hivyo hadi sasa.

Alimpongeza Dkt. Biteko kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Akizungumzia uhusiano mzuri ulipo kati ya Tanzania na China, aliishukuru Serikali ya Tanzania jinsi inavyoiunga mkono Serikali ya China katika majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Kwa upande wake, Dkt. Biteko aligusia maeneo ambayo Tanzania inahitaji ushirikiano kutoka China, ambayo ni kujengea uwezo wataalam kwenye masuala ya utawala pamoja na teknolojia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *