Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya China, imetoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya sh. milioni 100 kwa Serikali ya Tanzania kwa maendeleo ya michezo nchini.
Msaada huo umepokelewa leo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana wakati wa hafla ya kusaini ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa China nchini, iliyofanyika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza Balozi wa China nchini, Chen Ming Jian, amesema wametoa jumla ya mipira 1800 ikiwamo ya netiboli, kikapu na ya wavu huku jezi zikiwa 2634 .
Balozi huyo amesema sababu kubwa ya kutoa vifa vifaa vya michezo Tanzania ni kutokana na uhusiano mzuri wa nchi hizo.
“Tanzania ina vijana wenye vipaji ndiyo sababu ya kuleta vifaa hivyo, pia uhusiano mzuri baina ya nchi ya Tanzania na China,” amesema.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Balozi Dkt. Pindi Chana, amesema ziara za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimezaa matunda kwa kuendelea kupata ushirikiano na mabalozi wa mataifa mbalimbali ikiwamo China.
Amesema vifaa hivyo vya michezo vitasambazwa katika shule za mikoa ya Tanzania Bara na visiwani Zanzibar .
Ameeleza kuwa mpango ni kupeleka michezo mtaa kwa mtaa, vijiji, kata ili kuendeleza na kuinua michezo itakayosababisha kupata vipaji vya ndani na nje ya Tanzania.
“Tutaendelea kuhakikisha utamaduni, sanaa na michezo inaendelea kusonga mbele, kuboresha masuala ya michezo, tunataka kupeleka michezo kwa kila mtaa, ngazi za vijiji na kila kata na nasisitiza maeneo ya wazi yalindwe.
Ameongeza:” Tunaenda kuboresha mitaala yetu kwa kuweka somo maalum la michezo shuleni na kuwepo na mitihani kama ilivyo kwa masomo mengine”.