Chalamila ataka mwendokasi kufanya kazi saa 24, azindua mwendokasi Mbagala.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila ameyasema hayo leo Juni 27 wakati akizindua huduma ya usafiri wa magari yaendayo kasi kuelekea Kipindi cha maonesho ya Sabasaba 2023.

RC Chalamila ametumia usafiri wa gari la Mwendokasi kuanzia Gerezani karikaoo hadi mbagala Rangi tatu- Temeke ikiwa ni ishara ya Uzinduzi huo.

Aidha Mhe Chalamila amesema haoni sababu ya Mwendokasi DSM kutokufanya kazi masaa 24, ni dhamira yake kuona mabasi hayo yakifanya kazi masaa 24 ili kupanua wigo wa kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa.

Ndio maana Serikali iko mbioni Kuimarisha ulinzi kwa kuweka mifumo Stahiki ya Usalama ikiwemo taa na CCTV camera ili hata baadhi ya maeneo yenye masoko kama karikaoo huduma zitolewe masaa 24.

RC Chalamila amemshukuru Dkt Samia kwa kuendelea kutoa fedha nyingi ili kuboresha miundo mbinu ya Mwendokasi katika Mkoa huo na kuwataka DART kuwa wabunifu na kuboresha huduma za usafirishaji katika jiji hilo ikiwemo kero ya sasa ya abiria kukaa kwenye kituo kwa muda mrefu.

Hata hivyo Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa DART Ndg Deusdelity Casmir Mkurugenzi wa Fedha amesema kwa Kipindi chote cha maonesho ya Sabasaba kwa kushirikiana na TANTRADE tayari wanayo mabasi takribani 30 kwa kuanzia mabasi 20 yataanza kuhudumia wananchi hivyo wananchi wote wanakaribishwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *