Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Dar es Salaam, leo kitampokea Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Paul Makonda.
Mapokezi hayo yatafanyika katika Ofisi Ndogo za CCM zilizopo Lumumba, jijini Dar es Salaam, saa 3 asubuhi.
Hivi karibuni, Halmashauri Kuu ya CCM ilimteua Makonda kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi.
Uteuzi huo umefanyika baada ya Halmashauri Kuu ya Chama hicho kukutana Mjini Dodoma katika kikao chake maalum, chini ya Mwenyekiti Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na aliyekuwa Katibu NEC, Itikadi na Uenezi CCM Taifa, Sophia Mjema alisema; “Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imefanya mabadiliko madogo ya Sekretarieti ya halmashauri Kuu ya CCM Taifa.
“Halmashauri hiyo imemteua Paul Makonda kuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Taifa akichukua nafasi ya Mjema ambaye aliteuliwa kuwa Mshauri wa Rais Masuala ya Wanawake, Makundi Maalum.
Alisema Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pia imemteua Rabia Abdala Hamid kuwa Katibu wa Halamshauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), akichukua nafasi ya Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Uhusiano wa Afrika Mashariki.
Aliongeza kuwa, katika kikao hicho, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imezipongeza Serikali zake zote mbili ikiwemo ya Jamhuri ya Muungao chini ya Rais Dkt. Samia na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2020-2025.