Na Badrudin Yahaya
Kocha wa muda wa timu ya Simba SC, Daniel Cadena, amesema mapumziko ya wiki mbili yatawasaidia kurudi katika ubora wao.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Pulsesports baada ya kudondosha alama nyingine wakati walipolazimishwa sare ya 1-1 na Namungo FC kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Cadena ambaye ni kocha wa makipa, ameteuliwa kuziba nafasi hiyo kwa muda wakati viongozi wa klabu wakitafuta mbadala wa Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliyetimuliwa mapema wiki iliyopita baada ya kupokea kichapo cha mabao 5-1 kutoka kwa Yanga.
“Mapumziko yanayokuja mbele yetu yatakuwa na maana kwetu, wachezaji watapumzika kwa takribani siku tano na kisha kurejea kambini kwa ajili ya maandalizi,” amesema.
“Kutokana na matokeo yaliyopita na kisha kocha kuondoka ilikuwa ngumu kwetu kwa siku chache nilizopata kubadilisha kitu lakini baada ya mapumziko tutarudi tukiwa bora zaidi,” ameongeza.
Katika mchezo huo, Reliants Lusajo aliwatanguliza Namungo kwa bao la kwanza dakika ya 29 lakini Jean Baleke aliisawazishia Simba dakika ya 75.
Bao la Baleke lilikuwa ni la saba na sasa anaungana na Stephan Aziz Ki na Max Nzengeli wa Yanha ambao ndio walikuwa vinara wa mabao.
Sare hiyo inawafanya Simba kufikisha alama 19 wakisalia nafasi ya tatu kwakuwa wamezidiwa mabao na Azam mwenye alama 19 na Yanga alama 24.