Bunge laridhia mkataba Taasisi ya Dawa Afrika

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

BUNGE la Tanzania, jana limepitisha Azimio la mapendekezo ya kuridhia Mkataba wa Kuanzisha Taasisi ya Dawa Afrika ya Mwaka 2019 (AMA ).

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema katika utekelezaji wa AMA, upo uwezekano wa nchi kupata manufaa zaidi, kuimarika kwa mfumo wa udhibiti wa bidhaa tiba.

Lengo ni kudhibiti bidhaa ambazo kwa sasa hazijaanza kudhibitiwa kama viambata hai, damu, bidhaa zake, tiba za kijenetiki na chembe msingi.

Alieleza kuwa, AMA itaisaidia Tanzania kuongeza viwanda vya bidhaa tiba nchini na kuwasilisha taarifa kwa nchi wanachama wa AMA za kuomba usajili zenye vigezo vinavyofanana hivyo kupunguza usumbufu na muda wa kusajili bidhaa zao katika nchi hizo.

“AMA itasaidia kuimarika mifumo ya udhibiti wa bidhaa tiba duni na bandia, kuwezesha kukabiliana na bidhaa tiba zinazopitishwa kwa kutumia njia zisizo rasmi katika mipaka ya nchi jirani,” alifafanua Mwalimu.

Aliongeza kuwa, pia AMA itasaidia kukua kwa soko la bidhaa tiba za viwanda vya ndani kutokana na kuwianishwa masharti ya usajili wa bidhaa tiba kwa nchi wanachama kama ilivyo ainishwa katika Mkataba wa AMA.

Hata hivyo, alisema AMA itasaidia usajili, upatikanaji wa bidhaa tiba haraka, kupunguza gharama zinazotokana na taratibu za usajili wa bidhaa hizo kwa kuwianisha mifumo ya usajili na kuondoa utaratibu wa sasa ambapo kila nchi huhitaji kukagua viwanda vinavyozalisha bidhaa tiba miongoni mwa nchi wanachama wa AMA.

Pia itasaidia uimarishaji mifumo ya udhibiti wa bidhaa tiba duni na bandia miongoni mwa nchi wanachama wa AMA kutokana na kurekebishwa kwa mfumo wa kisheria wa nchi hizo kwa kuzingatia Sheria ya Mfano ya AU iliyopitishwa mwaka 2016

AMA itaharakisha upatikanaji wa bidhaa tiba hasa wakati wa dharura na majanga kutokana na kuwa na mifumo ya usajili iliyowianishwa

Alisema pia AMA itarahisisha kupata taarifa kwa urahisi kutoka kwa nchi mbalimbali zilizoridhia na zinazotekeleza Mkataba, kutambua umuhimu wa kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa kwa ufanisi ili kuimarisha uwezo wa nchi kudhibiti bidhaa tiba, kuhakikisha zinapatikana kwa haraka zikiwa zenye ubora, ufanisi na salama.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *