Bunge bonanza yafana, wananchi waaswa kutumia michezo kudumisha muungano

Na Sarah Moses, Dodoma

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdullah amewaasa watanzania kutumia michezo kudumisha muungano ,amani na mshikamano kwani ndio tunu ya Taifa la Tanzania.

Akizungumza leo Juni 22,2024, kwenye CRDB Bunge Grand Bonanza lililoandaliwa na Benki hiyo ambapo amesema watumishi wa serikali na Wabunge walitumie Bonanza hilo kuimarisha afya zao.

“Bonanza hili limefana sana na limenifurahisha niwapongeze sana bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maandalizi na niwasihi kuendeleza ushirikiano baina yenu na baraza la wawakilishi katika masuala mbalimbali kama hivi leo mlivyofanya katika bonanza hili,”amesema.

Pamoja na hayo amesema ushirikiano baina ya Bunge la Jamhuri ya Muungano Tanzania na Baraza la Wawakilishi Zanzibar uendelee hata katika masuala ya michezo.

Kwa upande wake Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzanja Dkt Tulia Ackson amesema bajeti mpya ya serikali imegusa wananchi moja kwa moja hasa wanamichezo kwa kutenga zaidi ya bil.280 .

” Fedha hizi zitatekeleza mambo mbalimbali kwenye sekta ya michezo lakini pia niwaombe wanamichezo kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan”amesema

Wakati huo huo Mkurugenzi wa Masoko na huduma kwa wateja Benki ya CRDB Tuli Mwampamba amesema lengo la kufanya matamasha ni kuwakutanisha viongozi wa serikali na wananchi huku akibainisha kuwa kuna ujio wa CRDB Marathon ambayo itafanyika Agosti 18,2024.

Aidha katika bonanza hilo kulikuwepo na michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu, mpira wa pete, Kufukuza Kuku, kupokezana vijiti, kula, kucheza bao kukimbia na magunia, mbio za riadha na michezo mingine.

Hata hivyo Pamoja na mambo mengine dhumuni kuu la bonanza hilo ni kuwezesha ujenzi wa shule ya sekondari ya Bunge wavulana (Bunge Boys) , kujenga afya na kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali
Lakini pia limehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati DKt.Doto Biteko.
Mwisho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *