Biteko: Samia ni mfano wa kuigwa

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amempongeza na kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kustawisha ustawi wa kidemokrasia nchini.

Pia alimpongeza kwa kuimarisha miundombinu ya kiuchumi, kijamii ili kuwaletea maendeleo Watanzania.

Dkt. Biteko alitoa pongezi hizo Dar es Salaam jana wakati akifunga Mkutano Maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini ukishirikisha wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili Miswada ya Sheria za Uchaguzi na Muswada wa Sheria za Vyama vya Siasa ulioandaliwa na Baraza la Vyama vya Siasa nchini.

Miswada iliyojadiliwa ni Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

“Rais wetu amekuwa mfano wa kuigwa, kitaifa, kimataifa kwa kuhakikisha demokrasia inazidi kustawi na kuifanya Serikali kuendeshwa kwa misingi ya haki, utawala bora na kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea.

“Pia serikali inazingatia maoni ya watu ambao ni muhimu katika kuboresha utendaji wetu,” alisema Dkt. Biteko.

Alilipongeza Baraza la Vyama vya Siasa kwa kuandaa mkutano huo ambao ni muhimu kwa maslahi ya Taifa.

Alisema baraza hilo kwa kwa mujibu sheria linajukumu la kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa sheria ya vyama vya siasa, masuala mengine yanayohusu vyama vya siasa na demokrasia.

Aliongeza kuwa, mkutano huo umekuwa wenye tija kwani washiriki wameweza kutoa maoni yao kwa kuzingatia maslahi ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko aliwaasa wajumbe wa Mkutano huo kuitikia wito wa Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson wa kwenda bungeni kuanzia Januari 6-10, 2024 ili kutoa maoni yanayohusu Miswada ya Sheria za Uchaguzi, Mswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa.

Aliwashukuru wajumbe hao kwa kutoa maoni ambayo ni bora, kujadiliana kwa uungwana kuhusu miswada hiyo, hakuna chama kilichoonesha kina umiliki wa kutoa mawazo bali wote walisikilizana.

Dkt. Biteko alisema yale waliyojadiliana itakuwa ni muendelezo wa kujenga maridhiano ya kitaifa.

Kuhusu sheria zilizopo nchini, alisema kama kuna sheria inaonekana ina changamoto baada ya kuitumia kwa muda mrefu, wito wa Dkt. Samia ni sote kukaa na kuridhiana kama Taifa wapi tuboreshe.

Bunge ni taasisi mahiri yenye uongozi mahiri ambao watapokea maoni yetu, kuyafanyia kazi, mahali ambapo Serikali itapaswa kupeleka Muswada wa Sheria ya marekebisho bungeni itafanya hivyo.

Awali Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama, alisema lengo la mkutano huo ni kukutanisha wadau wengi wanaohusika na masuala ya demokrasia ya mfumo wa vyama vingi nchini.

Lengo ni kutoa maoni yatakayoboresha miswada kupitia utaratibu utakaozingatia sheria na kanuni za upitishwaji wa Miswada katika Bunge la Tanzania.

Alisema mkutano huo umekuwa na mafanikio makubwa na wadau wametoa maoni yao kwa amani, ushirikiano mkubwa hivyo alilipongeza Baraza la Vyama vya Siasa, kwa kuandaa mkutano huo akisema Serikali itaendelea kuwaunga mkono katika utekelezaji wa mipango yake.

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi alisema zao la mkutano huo ni muongozo uliotolewa na Rais Dkt. Samia wakati akipokea taarifa ya kikosi kazi alichokiunda cha kuratibu maoni ya wadau wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa.

Moja ya masuala aliyoelekeza ni kufanyika maboresho ya sheria za uchaguzi na sheria za vyama vya siasa.

Alimshukuru Rais Dkt. Samia kwa jitihada zake za kukuza, kuendeleza demokrasia nchini kwani kukutana kwa Baraza hilo kunatokana jitihada za uwepo wa demokrasia nchini.

Viongozi mbalimbali waliohudhuria Mkutano huo ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hamza Hassan Duma, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *