Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, jana amewasilisha azimio la Tanzania kujiunga na Mkataba wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu- IRENA bungeni jijini Dodoma.
Katika wasilisho hilo, Dkt. Biteko alitaja manufaa mbalimbali yatakayopatikana baada ya kujiunga na mkataba huo.
Manufaa hayo ni pamoja na kuimarika kwa mchango wa nishati jadidifu katika uzalishaji nishati ya umeme nchini, kuliwezesha taifa kuwa na vyanzo mchanyanyiko vya umeme unaoendana na mahitaji ya ukuaji uchumi.
Alitaja manufaa mengine ni kuimarika kwa uwekezaji, mitaji, upatikanaji ushauri wa kiufundi katika uendelezaji nishati jadidifu na kupungua kwa uharibifu wa mazingira unaotokana na uzalishaji, matumizi ya nishati isiyo rafiki wa mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.