Biteko atoa agizo zito TPDC

*Ataka mpango upatikanaji gesi asilia

*Asisitiza ukaguzi ushuru wa huduma

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuja na mpango wa muda mrefu utakaoonesha jinsi nchi itakavyoweza kuongeza kiasi cha gesi asilia.

Lengo ni kuhakikisha muda wote kunakuwa na hazina ya  nishati hiyo ambayo itatumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemouzalishaji umeme kwenye magari, majumbani pamoja na viwandani.

Dkt. Biteko aliyasema hayo jana wakati wa kikao chake na Bodi, Menejimenti ya TPDC kililenga kufahamiana,
kubadilishana mawazo kuhusu utendaji kazi akitumia fursa hiyo kuelekeza matarajio ya nchi kutoka TPDC.

“TPDC tujiulize, je, uwezo wetu wa kuzalisha gesi asilia unaweza kujibu mahitaji yetu ya gesi ? tujiulize hili na tuchukue hatua, tambueni kuwa mahitaji ya gesi asilia ni makubwa kwa sasa, dunia inahama kutoka matumizi ya mafuta kwenda katika gesi asilia, lazima tujipange.

“Tumesaini makubaliano ya kusafirisha nishati hii kwenda Uganda, Zambia na Kenya hivyo lazima tuwe na gesi ya kutosha,” alisisitiza Dkt. Biteko

Aliwataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji
maamuzi mbalimbali hususan katika utafiti wa mafuta, gesi asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake katika Kisiwa cha Songosongo, mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati, mkoani Mtwara, Dkt. Biteko amesisitiza maisha ya wananchi katika maeneo lazima yabadilike, wapewe huduma bora ikiwemo maji, afya, umeme pamoja na usafiri.

“Nashukuru mmeanza kuyafanyia kazi maagizo ambayo niliyatoa ikiwemo kuweka taa za barabarani Kijiji cha Msimbati, kupeleka umeme wa uhakika Madimba na Msimbati unaotoka kwenye mitambo ya gesi asilia.

“Pia kupeleka kivuko Kisiwa cha Songosongo, malipo ya mafao kwa wastaafu wa Knight Support ambao walikuwa wakilinda mitambo na visima vya gesi asilia Songosongo ambao hawakulipwa muda mrefu, watu hawa
wanahitaji huduma bora,” alisema.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameiagiza TPDC kupita kwenye halmashauri zote nchini zinazopokea ushuru wa huduma kutokana na shughuli za mafuta, gesi asilia ili wajiridhishe kama fedha hizo zinaenda vijijini na maeneo ambayo shughuli za uzalishaji gesi asilia zinafanyika.

Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame alimweleza Dkt. Biteko kuwa TPDC inaandaa Mpango Mkakati wa Shirika (Corporate Strategic Plan) ambao utaweka mikakati ya Shirika kwa kipindi cha miaka 10.

Lengo ni kuwezesha upatikanaji wa gesi asilia ya kutosha kwa matumizi ya ndani, kuwekeza zaidi katika mnyororo wa thamani wa mafuta na gesi ili kukuza matumizi ya gesi asilia hivyo kuchochea biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Alieleza mipango ya utekelezaji mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Uganda kuja Tanzania, Mradi wa Gesi ya Kusindika (LNG), majadiliano yamekamilika, mikataba ipo kwenye hatua za kuidhinishwa, utafutaji  mafuta na gesi asilia katika Kisiwa cha Songosongo Magharibi unaotarajiwa kuanza Septemba, 2025 na utafutaji mafuta kitalu cha Eyasi Wembere, tafiti zinaendelea.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TPDC, Balozi Ombeni Sefue, alimshukuru Dkt. Biteko kwa maelekezo yake ambayo yamewapa hamasa ya kufanya kazi na kuahidi kuwa, wataenda mbali zaidi kiutendaji
na watampa ushirikiano ili kusukuma maendeleo zaidi katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *