Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetoa mkopo wa zaidi ya sh. bilioni 44.2 kwa wanafunzi wapya 14,428 awamu ya pili waliopangiwa mikopo walioomba kwa mwaka wa masomo 2023-2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na bodi hiyo mwishoni mwa wiki, ilisema wanufaika ni wanafunzi wote waliopo awamu ya pili na wapya wanaojiunga na masomo ya Shahada ya kwanza katika taasisi za elimu ya juu mbalimbali zilizopo nchini.
Ilieleza kuwa, hadi sasa wanafunzi 70,560 wapya wa mwaka wa kwanza wamepangiwa mikopo yenye thamani ya sh. bilioni 203.9.
“Itakumbukwa wanafunzi 56,132 wa Shahada ya Kwanza walipangiwa mikopo ya sh. bilioni 159.7 katika Awamu ya Kwanza (Batch I) iliyotangazwa Oktoba 20, 2023.
“Kati ya wanafunzi 70,560 waliopangiwa mikopo hadi sasa, wanaume 40,470 sawa na asilimia 57.3, wanawake 30,090 sawa na asilimia 42.6,” ilieleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua, wanafunzi waliopangiwa mikopo Awamu ya Pili kama ilivyo kwa waombaji wote, wanapata taarifa za mikopo waliyopangiwa kupitia SIPA-Student’s Individual Permanent Account ambazo walitumia kuomba mkopo.
“Tunawakumbusha waombaji mkopo, SIPA ndiyo sehemu muhimu ya kupata taarifa za mwombaji kuhusu ombi lake la mkopo,” ilieleza.
Awamu ya Tatu (Batch III) ya mwisho itatolewa kabla ya Novemba 3, 2023 baada ya kukamilishwa uchambuzi wa mwisho wa maombi unaoendelea.
Baada ya Awamu ya Tatu, waombaji mkopo watapata fursa ya kuwasilisha rufaa ili kufikiriwa kupangiwa mkopo au kuongezewa baada ya kuwasilisha nyaraka za ziada.
Hata hivyo, Serikali imetenga sh. bilioni 731 kwa wanafunzi wa Shahada ya kwanza mwaka 2023/2024 kwa ajili ya wanafunzi 220,376 ambapo kati yao, wanafunzi 75,000 watakuwa ni wanufaika wa mwaka wa kwanza.