betPawa yatumia mil. 69.3/- ujenzi wa Zahanati ya Nangoma mkoani Mtwara

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

KAMPUNI ya Michezo ya Kubashiri ya betPawa, imetumia jumla ya sh. milioni 69.3 kukamilisha ujenzi na uboreshwaji wa zahanati ya kijiji cha Nangomba ya mkoani hapa.

Fedha hizo zimetumika katika ujenzi, uboreshaji na upanuzi wa zahanati hiyo kupitia programu ya ‘Dream Maker’ yenye lengo la kusaidia kutatua changamoto mbalimbali katika jamii nchini.

Kwa mujibu wa Meneja Masoko Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya betPawa, Borah Ndanyungu, wanajisikia fahari kushiriki katika jamii hasa sekta ya afya na kutatua tatizo hilo kwa Kijiji cha Nangomba.

Ndanyungu amesema hatua ya kuboresha zahanati imetokana na maombi yaliyowasilishwa na Ofisa Tabibu, Anania Muba kupitia program ya ‘Dream Maker’ ambayo hadi sasa imetatua changamoto mbalimbali 20 katika jamii.

“Uboreshwaji huo ni pamoja na kukarabati kuta zilizoharibika, kuinua urefu wa jengo, kuongeza mihimili na kumalizia kupiga plasta, kuweka milango, tiles, kupaka rangi kuta na kufunga madirisha ya kisasa ya aluminum,” amesema Ndanyungu.

Amesema Muba aliwasiliana na betPawa kupitia mradi huo akitafuta usaidizi katika kukamilisha ukarabati wa kituo cha umma baada ya maendeleo yake kukwama.

“Mpaka zaidi ya sh. milioni 500 zimetumika kusaidia jamii kupitia program ya Dream Maker na fedha hizo zimetumika kwa miezi 10. Programu ya Dream Maker ni mkakati wa kampuni yetu katika kusaidia jamii,”

“Ni ndoto za upendo kama hizi zinazotuhamasisha na kuendesha mradi wa Dream Maker kwa sababu tunajua kwamba pamoja tunaweza kuleta mabadiliko ya kudumu na chanya kwa kila jamii kwa wakati mmoja,” amesema.

Kwa upande wake, Muba amesema ndoto yake kubwa ilikuwa kukamilisha ukarabati na upanuzi wa kliniki yao ambayo inatoa huduma kwa wakazi zaidi ya 9,785.

“Jengo tulilokuwa tukilitumia hapo awali lilikuwa katika hali mbaya na halikuwa salama kutumika kama kituo cha afya. Nashukuru betPawa kwa kufanya ndoto yangu kuwa kweli kwa kukubali ombi langu ndani ya muda mfupi. Wakazi wa Ndangoma na maeneo jirani kwa sasa wanaweza kufurahia huduma katika mazingira ya kisasa, salama na ya usafi,” amesema Muba.

Kwa upande wake, Diwani wa Nangomba, Sijaona Athumani, ameipongeza Kampuni ya betPawa kwa kufanikisha mradi huo kutoa wito kwa kampuni mbalimbali kuiga mfano wa kamupuni hiyo kwa changamoto katika jamii bado ni nyingi.

“Nifuraha kuweza kuona zahanati hii itahudumia idadi ya wananchi wasiopungua 9,785 wakitokea sehemu mbalimbali hapa kijijini. Naishukuru betPawa kwa kutufanikishia ujenzi na uboreshwaji wa kituo hiki. Muba ameonyesha uzalendo wake kwa wakazi wa Ndangoma, naomba kila mmoja aige mfano wake,” amesema Athumani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *