Na Mwandishi Wetu
MPIRA wa kikapu nchini Tanzania, umeingia kwenye msimu mwingine wa ukuaji na maendeleo ya wachezaji baada ya betPawa kuendeleza rasmi udhamini wake wa Ligi ya Taifa ya Mpira wa Kikapu (NBL), ikiwa na uwekezaji mpya wa jumla ya sh. 317,025,900 kwa msimu huu.
Udhamini huo mpya unaendeleza mpango wa Locker Room Bonus (LRB), mfumo wa kipekee wa motisha unaotoa sh. 140,000 papo hapo kwa kila mchezaji baada ya kila ushindi kwenye mechi, kuhakikisha wachezaji wanahisi thamani ya mchango wao mara moja baada ya mchezo.
Locker Room Bonus imepata sifa kubwa barani Afrika kwa kubadilisha namna wachezaji wanavyojihusisha na mashindano, kwa kuwazawadia kwa jitihada zao na kuongeza kiwango cha ushindani.

Athari zake zilionekana wazi Tanzania wakati wa michezo ya mtoano msimu uliopita, ambapo uliwaongezea nguvu na ari wachezaji na timu.
Kupitia mkataba huo mpya, betPawa pia imetenga sh. milioni 13 kwa ajili ya tuzo za timu na wachezaji, ikiwemo tuzo za Mchezaji Bora (MVP), Mfungaji Bora na nyinginezo zinazolenga kutambua nyota wa msimu.
Akizungumzia kuhusu kuendelezwa kwa udhamini huo, Mkuu wa Masoko ya Ndani na CSR wa betPawa, Borah Ndanyungu, amesema: “Tunajivunia kuendelea kuunga mkono mpira wa kikapu hapa Tanzania. Locker Room Bonus imeonekana kuwa chachu kubwa ya motisha kwa wachezaji na udhamini huu unaonyesha imani yetu ya muda mrefu katika kukuza mchezo huu. Tunazingatia kuthamini juhudi, kuhamasisha vipaji na kuhakikisha kila ushindi una maana kwa wale wanaoufanyia kazi.”

Viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) wameukaribisha udhamini huo, wakibainisha kuwa betPawa inaendelea kuweka viwango vipya katika ustawi wa wachezaji, motisha na ushirikishaji wa mashabiki.
Ushirikiano huo pia unaimarisha nafasi ya Tanzania ndani ya ajenda ya maendeleo ya michezo barani Afrika ya betPawa, inayojumuisha kuunga mkono ligi na mashirikisho katika nchi mbalimbali kupitia ubunifu unaoweka mbele maslahi ya wachezaji na jamii.
