Na Rashid Abdallah, BBC
IJUMAA Mei 12, 2023, majira ya saa tano za asubuhi, taarifa ya kifo cha mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania, kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), ndipo zilipoanza kusambaa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Amefariki asubuhi katika hospitali ya Kairuki, Mikocheni jijini Dar es Salaam, baada ya kupelekwa alfajiri ya leo. Msaidizi wa Membe, Allan Kiluvya alieleza kwa vyombo vya habari kuwa alipata changamoto ya kifua.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kupitia mtandao wa Twitter alimwelezea marehemu alikuwa mtumishi mahiri wa umma, mwanadiplomasia, Mbunge na Waziri aliyeitumikia nchi kwa weledi.
Alivyoihudumia CCM na Tanzania
Baada ya kumaliza masomo ya juu nchini Marekani mwaka 1992, Membe alipewa kazi ya kuwa mshauri katika Ubalozi wa Tanzania, huko Ottawa nchini Canada, kutoka mwaka huo hadi 2000.
Membe ni mwanachama mkogwe wa CCM, aliyepata kukitumikia chama hicho katika nafasi ya Ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwongo mmoja na nusu, kutoka mwaka 2000 hadi 2015.
Kufuatia uchaguzi mkuu wa 2005, uliomuweka madarakani Rais wa nne wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete; Membe aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani. Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri ya Oktoba 2006, yakamuhamisha na kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Nishati na Madini.
Chini ya serikali hiyo hiyo, Membe akashika nyadhifa kubwa zaidi, pale alipoteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, akichukua kijiti hicho kutoka kwa Asha-Rose Migiro aliyekuwa ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Alikaa katika nafasi hiyo kutoka 2007 hadi 2015.
Membe alipata kushika wadhifa wa Uenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Umoja wa Afrika, mwaka 2008. Pia, alikuwa mkuu wa waangalizi wa uchaguzi mkuu wa Zimbabwe mwaka 2013, kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Nje, Tanzania ilifungua balozi katika nchi mbali mbali ulimwenguni. Pia, Tanzania ilipokea viongozi wakubwa ulimwenguni kama Rais wastaafu wa Marekani George W. Bush, Barack Obama, Xi Jinping (China) na Jacob Zuma (Afrika Kusini).
Mbio za urais na mvutano ndani ya CCM
Membe alikuwa miongoni mwa makada wa CCM alioingia katika kinyang’anyiro cha kutafuta ridhaa ya chama hicho kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2015. Jina lake likawa miongoni mwa yaliyokatwa na kupitishwa jina la hayati John Pombe Magufuli.
Kabla ya hapo kulikuwa na mvutano mkubwa wa nani atachukua nafasi hiyo kutokana na kambi mbili za wanaCCM wenye nguvu – Edward Lowassa na Bernard Membe mwenyewe. Mvutano huo ulilazimisha Chama ‘kiwafunge kufuli’ makada kadhaa, wakiwemo Membe na Lowassa, kufanya kampeni zozote kabla ya wakati na kwamba walikuwa hatarini kusimamishwa na hata kufutwa uanachama.
Kukosa nafasi ya kuiwakilisha CCM kukawa ndio mwanzo wa mwanasiasa hiyo kuingia katika mvutano na chama chake na kuonekana kana kwamba anamtunishia misuli Rais Magufuli. Na hilo halikuishia vizuri.
Februari 2020 alifukuzwa uanachama na CCM, kupitia Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, akituhumiwa kukiuka miiko na katiba ya chama.
Mwenyewe alikana tuhuma hizo na kusema alifukuzwa kwa kuwa alitaka kugombea na kushindana na Magufuli ili ateuliwe kuiwakilisha CCM katika ngazi ya urais.
Membe alijiunga na ACT Wazalendo Julai 2020, na kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huo, na kupata asilimia 0.5 ya kura zote. Uchaguzi ambao ulimrudisha Magufuli wa CCM madarakani.
Membe alijiuzulu ACT Januari 2021. Na ilipofika Mei 2022 alirejeshewa uanachama wake na CCM, baada ya CCM kueleza kuwa aliomba radhi zaidi ya mara moja. Hadi mauti yanamkuta, Bernard Membe ni mwanachama cha CCM.
Alikotoka
Barnad Kamilius Membe amefariki akiwa na miaka 69 – alizaliwa Novemba 9, 1953, Rondo, Chiponda mkoani Lindi, wakati huo Tanganyika ambayo sasa ni Tanzania ikiwa chini ya himaya ya Mkoloni, Mwingereza.
Alianza kupata elimu yake ya msingi mwaka 1962, katika shule ya Chiponda, Lindi. Elimu ya sekondari aliipata shule ya Namupa Seminary, Lindi. Sekondari kidato cha tano na sita aliipata Itaga Seminary, Tabora.
Membe alisoma sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nchini Tanzania. Alijiendeleza kielimu, katika chuo kikuu cha Johns Hopkins, nchini Marekani katika fani ya Uhusiano wa Kimataifa kati ya 1990 na 1992.
Membe ameacha mjane mmoja na watoto watatu.