Na Mwandishi Wetu, Mbeya
BENKI ya Letshego Faidika, imetumia jumla ya sh. 5,348,067,950.91 kukopesha wateja 1,305 wa mkoani hapa.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Bodi ya Benki ya Letshego Faidika, Adam Mayingu wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la benki hiyo maeneo ya Soweto mkoani Mbeya.
Awali tawi hilo lilikuwepo kwenye Jengo la Royal Zambezi kabla ya kuhamia Soweto, karibu na barabara ya Moondust.
Mayingu amesema kiasi hicho cha fedha kimekopeshwa kwa wateja wao mbalimbali serikalini na sekta binafsi.
Amesema Benki ya Letshego Faidika ni matokeo ya muungano kati ya taasisi ndogo ya kifedha, Faidika na Benki ya Letshego Tanzania ambayo ilianza kufanya kazi Julai Mosi, mwaka jana.
Amesema tawi hilo lina historia ya kipekee ambapo kwa upande wa Benki ya Letshego ilianza kutoa huduma mwaka 2016 na kwa upande wa Faidika ilianza kutoa huduma mwaka 2008.
“Hadi sasa tumeweza kuwahudumia wateja zaidi ya 3,417 kwa Mkoa wa Mbeya pekee. Pia, tuna satellite 6 ambazo ziko Ileje, Mkwajuni, Mbarali, Tukuyu, Kyela, na Mbozi. Tunajivunia sana, kwani linaleta uthibitisho wa dhamira yetu ya kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi Mbeya na mikoa mengine,”amesema Mayingu.
Amesisitiza huduma za benki hiyo zinalenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kutoa suluhisho la kifedha kwa watumishi wa umma, wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo na wa kati na huduma nyingine kama mikopo ya magari, akaunti za akiba na bima.
“Kauli mbiu yetu, “Tunaboresha Maisha,” inaendelea kuimarisha dhamira yetu ya kuwa washirika wa kweli wa maendeleo. Kwa mara nyingine tena, napenda kutoa pongezi za dhati kwa timu ya Letshego Faidika kwa kazi kubwa ya kuandaa uzinduzi huu,” amesema Mayingu na kuongeza.
“Pia, niwashukuru washiriki wote wa kikundi kazi kilichoshiriki kuhakikisha kuwa uzinduzi huu unafanikiwa. Tunatarajia kuendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuhakikisha huduma bora na zenye tija zinaendelea kupatikana hapa Mbeya.
Kwa upande wake, Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa ameipongeza benki hiyo kwa kufungua tawi hilo huku akiiomba kuongeza matawi zaidi mkoani humo na mikoa ya jirani.
Malisa amesema Mbeya ni mlango wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na ni fursa kwa benki hiyo kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika mikoa ya kusini.
Amesema asilimia 95 ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya ni wafanyabiashara ambapo endapo benki ya Letshego Faidika ikiwatumia vizuri, watapata faida kubwa.
Malisa pia ametoa wito kwa viongozi wa benki hiyo kuendelea kupanua wigo wa huduma kwa kufungua matawi zaidi, ili kuwafikia wateja zaidi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika mkoa wa Mbeya.
Wakati huo huo, Mkurugenzi wa Benki Kuu tawi la Mbeya, Dkt. James Machemba, ameipongeza benki hiyo kwa huduma bora za kifedha nchini na pia kuendelea kupanua wigo wa huduma za kibenki.
Amesema kufungua tawi mkoani humo, kuleta ushindani na benki nyingine ili kuwapa chaguo wateja.