Na Mwandishi Wetu
BENKI ya CRDB, imezindua rasmi msimu mpya wa mashindano ya soka na netiboli yajulikanayo kwa jina la CRDB Bank Supa Cup 2024.
Uzinduzi huo umefanyika mkoani Dodoma kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya John Merlin na Mkuu wa Fedha wa benki hiyo, Fredrick Nshekanabo, pamoja na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Nshekanabo alisema lengo kuu la mashindano hayo ni kuongeza ari, nguvu na ushirikiano baina ya wafanyakazi wa benki.
“Baada ya kusambaza tabasamu kwa wananchi wa Tanzania na kuvuka mipaka ya nchi na kwenda nchini DR Congo na Burundi, sasa ni zamu ya tabasamu hilo kurudi nyumbani kwa wafanyakazi,” alisema Nshekanabo.
Alisema mashindano hayo yatashirikisha wafanyakazi wa Benki ya CRDB kutoka matawi mbalimbali, pamoja na makao makuu wakishindana vilivyo kugombania kombe la msimu.
Aidha, mashindano hayo yalienda sambasamba na programu ya kujitolea kwa wafanyakazi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugeni wa Rasilimali Watu walitoa misaada ya vifaa vya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, kuchangia damu, pamoja na kutoa chakula na vinywaji kwa wagonjwa wa hospitali hiyo.
Benki ya CRDB ilianzia programu hiyo maalumu ya wafanyakazi wake kujitolea mwaka huu ikilenga kusogea karibu kwa jamii wanayoihudumia.
Kwa upande wake, Rutasingwa alisema benki yao ni sehemu ya jamii na ndiyo maana wamekuwa mara kwa mara wakishiriki katika programu za kusaidia jamii.
Programu hiyo ilizinduliwa visiwani Zanzibar mwezi uliopita na inatarajia kuendelea kufanya hivyo katika mikoa mingine baada ya Dodoma.