Benchikha arithi mikoba ya Robertinho Simba SC

Na Badrudin Yahaya

Klabu ya soka ya Simba, imemtangaza Abdelhak Benchikha kuwa kocha mpya wa kikosi hicho akiziba nafasi iliyoachwa wazi na Roberto Oliveira ‘Robertinho’.

Kocha huyo raia wa Algeria, ana uzoefu mkubwa wa kufanya kazi katika ngazi juu katika soka la Afrika.

Anajiunga na Simba akiwa anatokea katika klabu ya USM Alger ambayo msimu uliopita aliwasaidia kushinda taji la Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuwafunga Yanga katika mchezo wa fainali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Klabu hiyo, msimu huu Benchikha ameisaidia USM Alger kushinda ubingwa wa Super Cup ambapo aliwafunga Al Ahly katika mchezo uliofanyika Saudi Arabia.

Ameachana na miamba hao wa Algeria mwanzoni tu mwa msimu baada ya kushindwa kuelewana na viongozi katika baadhi ya mambo.

Simba kesho wanashuka dimbani kucheza na Asec Mimosa katika mchezo wa kwanza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, kocha Benchikha hatakuwa sehemu ya benchi la ufundi na badala yake Kaimu Kocha, Daniel Cadena ataendelea na majukumu yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *