BERLIN, Ujerumani
KAMA ndio timu ya Bayern Munich, imeanza kwa ushindi wa mabao 27-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Rottach-Egern kujiandaa na msimu mpya, haina haja ya kumsajili straika, Harry Kane.
Wachezaji 13 ndio waliofunga mabao hayo huku Jamal Musiala, Mathys Tel na Marcel Sabitzer kila mmoja akifunga mabao matano.
Sabitzer ambaye alikuwa kwa mkopo Manchester United msimu uliopita, alifunga mabao yake matano katika dakika 22 za kipindi cha pili.
Hadi kufikia mapumziko, Bayern ilikuwa ikiongoza kwa 18-0 kabla ya timu hiyo ya ridhaa Rottach-Egern kuongezwa mengine mabao 9 kipindi cha pili.
Mchezaji mwingine Serge Gnabry alifunga mabao matatu, Alphonso Davies, Konrad Laimer, Noussair Mazraoui, Dayot Upamecano, Leroy Sane, Raphael Guerreiro, Ryan Gravenberch, Kingsley Coman na Sadio Mane, pia walifunga.
Bayern ambayo imekuwa ikihusishwa na kumsajili Kane kipindi hiki cha usajili, iliichapa timu hiyo 23-0 mwaka 2019.