*Amng’oa bosi wa miradi Mhandisi Mkumbo
Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amesema baadhi ya wataalam, wasimamizi wa miradi ya barabara kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) hawatekelezi wajibu wao kikamilifu.
Hatua hiyo husababisha miradi mingi ya barabara nchini kutokamilika kwa wakati na viwango vinavyotakiwa
Bashungwa aliyasema hayo mkoani Tanga wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Mkange-Tungamaa- Pangani yenye urefu wa Km 120.8.
Barabara hiyo inatekelezwa na Mkandarasi, China Railway 15 na kusema hajaridhishwa na usimamizi wa mradi huo ambao upo nyuma kwa asilimia 19.2.
Alisema tayari ameanza kuchukua hatua kwa wataalam ambao ni chanzo cha miradi kutotekelezwa kwa wakati kulingana na mikataba kwa kumuondoa Mkurugenzi wa Miradi TANROADS, Mhandisi Boniface Mkumbo.
“TANROADS niliwaambia, nileteeni orodha ya barabara zote ambazo utekelezaji wake unasuasua hamkuleta, sasa unajua kwanini nimemfukuza MhandisiMkumbo, alikuwa sehemu ya kusababisha haya,” alisema Bashungwa.
Alimtaka Kaimu Mkurugenzi mpya wa Miradi, Mhandisi John Malisa kuzungukia miradi yote ya barabara nchini, kumletea taarifa ya miradi inayosua sua ili aweza kuchukua hatua.
Pia alimuagiza Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohammed Besta kuhakikisha kila mradi unaotekelezwa uwe na Msimamizi na Meneja.
Viongozi hao wawe katika katika maeneo ya miradi hiyo wakati wote hadi mradi utakapokamilika.
“Gharama za ucheleweshwaji ujenzi wa barabara ni kubwa kiuchumi kwa maendeleo ya wananchi, Serikali haitamvumilia Mkandarasi atakayeshindwa kutekeleza mradi kwa wakati kulingana na mkataba,” aliongeza.
Bashungwa amemuagiza Mhandisi Besta kufanya usanifu wa kina wa barabara ya Mkata-Kwamsisi yenye urefu wa 36, ifikakapo Desemba 31,2023 iweze kutengewa bajeti ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Naye Mhandisi Besta alimuhakikishia Bashungwa kuwa, maelekezo yake yatafanyiwa kazi ili kukamilisha miradi inayoendelea na kujenga miradi mipya.