Na Mwandishi Wetu, Tanga
WAZIRI waUjenzi, Innocent Bashungwa, amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mhandisi Mohammed Besta kukamilisha usanifu wa kina wa Barabara ya Mkata-Kwamsisi Km 36, ifikapo Desemba 31, mwaka huu.
Bashungwa alitoa agizo hilo jana alipofanya ziara ya kukagua athari za mvua za vuli mkoani Tanga.
Alisema fedha za mradi huo zipo tayari, kinachotakiwa kazi ya usanifu ifanyike ili ujenzi uanze mara moja.
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameashatoa fedha za ujenzi wa barabara hii hivyo kazi ya usanifu ikikamilika ujenzi uaanze haraka,” alisisitiza Bashungwa.
Alizungumzia umuhimu wa watendaji wa TANROADS katika ngazi zote kushirikiana na Mamlaka za Serikali ya mitaa ili kurahisisha ufuatiliaji kazi za Wakandarasi na kuwezesha kufutilia haki za watumishi katika miradi ya ujenzi hivyo kuleta tija katika utekelezaji wake.
Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Besta alisema wamejipanga kuhakikisha usanifu unakamilika kwa wakati, taratibu za kumpata Mkandarasi wa ujenzi huo unakamilika mapema iwezekanavyo.