Na Badrudin Yahaya
Kocha Mganda, Mosses Basena, ametimuliwa ndani ya timu ya Ihefu FC ikiwa zimepita siku 50 tangu apewe kibarua cha kuinoa timu hiyo kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
Basena alitangazwa kuwa kocha mpya wa timu hiyo Oktoba 16 kurithi mikoba ya Zuberi Katwila aliyejiunga na Mtibwa Sugar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kupitia mtandao wao wa Instagram, imeonesha wakimshukuru kocha huyo bila kueleza zaidi kwa kina.
Mara ya mwisho Basena aliiongoza timu hiyo juzi katika mchezo dhidi ya Tanzania Prisons ambao ulimalizika kwa suluhu.
Kocha huyo kwa ujumla ameiongoza timu hiyo katika mechi saba ambazo sare ni nne na alifungiwa mechi 3 huku akiicha timu hiyo katika nafasi ya 14 kwa pointi 10.
Awali kabla ya kocha huyo kutimuliwa, uongozi wa klabu ya Dodoma Jiji, umetangaza kuvunja mkataba na Melis Medo kwa madai ya kocha huyo anahitaji kushughulikia changamoto zake za kifamilia.
Kocha huyo raia wa Uingereza, alijiunga na Dodoma Jiji mwanzo wa msimu huu ambapo hapo awali aliwahi kuifundisha timu ya Coastal Union ya mkoani Tanga katika msimu wa 2020-21.
Kabla ya taarifa kutoka katika uongozi wa Dodoma Jiji kocha Medo hajaonekana kwenye benchi la timu hiyo katika michezo mitatu mfululizo ambayo timu yake imeambulia kichapo kwenye mechi zote tatu.
Kwasasa timu ipo chini ya kocha msaidizi Kassim Lyogope ambaye amekuwa nayo katika mechi zilizopita na anakiandaa kikosi hicho kuelekea mechi yao ya Desemba 18 dhidi ya timu ya Ihefu.
Timu nyingine ambazo zimeshaachana na makocha wao ni Singida FG ambao wamefukuza makocha wawili, Simba, Namungo, Mtibwa Sugar, Ihefu imetimua makocha wawili, Coastal Union na Tanzania Prisons.