Na Badrudin Yahaya
Mabao mawili yaliyofungwa na mastraika Jean Baleke na Mosses Phiri, yameiwezesha timu yao ya Simba SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Ihefu FC katika mfululizo wa mechi za Ligi Kuu Bara.
Ushindi huo, umeifanya Simba kufikisha alama 18 sawa na vinara Yanga ila zinatofautiana kwa mabao na kuifanya ibaki nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo.
Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, ulikuwa kama wa upande mmoja kwa baadhi ya nyakati kutokana na muda mwingi Ihefu kucheza nyuma ya mpira na mbele kuacha mchezaji mmoja.
Pamoja na mfumo huo uliokuwa ukitumiwa na Kocha mpya wa timu hiyo, Mganda Mosses Basena, Simba iliwachukua dakika 12 kufunga bao la kwanza kupitia kwa Mkongo Baleke ikiwa hilo ni bao lake la sita msimu huu katika ligi hiyo.
Baleke alifunga bao hilo kwa shuti nje ya eneo la hatari baada ya kuunasa mpira uliorudishwa vibaya na beki, Vedastus Mwihambi na kuunasa na kupiga shuti hilo huku Kipa, Fikirini Bakari akiruka bila mafanikio.
Baada ya kufungwa bao hilo, Ihefu ilionekana kama kufunguka kidogo na kushambulia kwa kushtukiza ambapo Ismail Mgunda aliisawazishia timu yake dakika ya 25 akimalizia mpira uliotemwa na Kipa, Ally Katoro akipangua shuti la Never Tigere.
Licha ya Simba kuendelea kuliandama lango la Ihefu muda wote, hadi timu hizo zikienda mapumziko zilifungana bao 1-1.
Baada ya mapumziko, Kocha alimtoa Baleke na kumuingiza Phiri ambaye ndio alikwenda kufunga bao la ushindi dakika ya 65 kwa kuitumia vizuri pasi ya Luis Miquisonne ambaye naye aliingia kipindi cha pili akichukuwa nafasi ya Kibu Denis.
Simba sasa itaingia mawindoni kujiwinda kucheza dhidi ya Yanga kwenye mechi ambayo itachezwa Novemba 5 kwenye Uwanja wa Mkapa.