Na Badrudin Yahaya
KIUNGO mshambuliaji wa timu ya Yanga SC, Stephan Aziz KI, ameifungia bao pekee timu yake katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Tabora United kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Bao hilo la pekee limefungwa kwa njia ya mpira wa adhabu ndogo dakika ya 21 ya mchezo na kuwafanya ‘wananchi’ kuhitimisha mechi zao ndani ya mwaka huu kwa ushindi muhimu.
Ushindi huo, umeifanya Yanga kujisogeza nyuma ya Azam baada ya kufikisha alama 30 ikiwa ni alama moja tofauti na vinara wa ligi hiyo.
Kwa kiasi kikubwa mchezo huo, ulitawaliwa na undava na nguvu nyingi huku timu zote zikikosa utulivu wa kuweka mpira chini.
Aziz Ki angeweza kufunga bao lingine kwa njia ya faulo kama sio uimara wa kipa wa Tabora United, John Noble ambaye alipangua mpira huo ambao ulikuwa unajaa kambani.
Bao alilofunga Aziz KI, limemfanya kufikisha idadi ya mabao 10 na kuendelea kujikita kileleni kwenye orodha ya wafungaji bora msimu huu.
Nyota wengine wenye mabao mengi ni Jean Baleke wa Simba pamoja na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC, ambao kila mmoja ana mabao 8.
Kiungo wa Yanga, Maxi Nzengeli ameganda kwa muda mrefu akiwa na mabao 7 katika nafasi ya tatu sawa na Waziri Junior wa KMC.