Na Samson Sombi
BAADA ya kupata Uhuru wa nchi yetu mwaka 1961, Mwalimu Julius Nyerere alitangaza vita nyingine ya kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao aliwataja kuwa ni ujinga, Umaskini na maradhi. Vita hii ilipiganwa na kila mwananchi ili kujikomboa kiuchumi.
Ili kufanikisha yote hayo, Mwalimu Nyerere alianzisha vijiji vya ujamaa kwa lengo la kuweka wananchi pamoja ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji na nyinginezo.
Katika vijiji hivyo kulitekelezwa sera ya siasa ya ujamaa na kujitegemea kwa kuanzisha mashamba ya ujamaa maduka, vyama vya ushirika ufugaji na biashara ndogo ndogo pia zilijengwa zahanati kwa ajili ya wananchi kupata matibabu.
Katika hatua ya kupambana na maadui wa maendeleo ulianzishwa mfumo wa Elimu ya Msingi kwa Wote (UPE). Kila mtoto mwenye umri wa kuanza shule alipelekwa shule ingawa mwitikio wake ulikuwa hafifu sana kwa wakati huo.
Ujamaa na Maendeleo Vijijini, sera hii ilisisitizwa na kutolewa mwongozo zaidi katika Azimio la Arusha lililoanzishwa Februari 5, 1967. Pamoja na mambo mengine, Azimio la Arusha lililenga kuleta ukombozi hasa vijijini wananchi kumiliki ardhi na kuimarisha shughuli za uzalishaji mali.
Serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya uongozi wa Mwalimu Nyerere ilianzisha Azimio la Iringa la ‘Siasa ni Kilimo’ mwaka 1972. Madhumuni ya kuanzishwa kwake ilikuwa ni kuboresha maisha ya wakulima kwa kupeleka wataalamu wa kilimo vijijini, pembejeo na kuwatafutia wakulima masoko ya mazao yao.
Idadi kubwa ya watanzania huishi vijijini na kujishughulisha na shughuli za kilimo, Ufugaji, Uchimbaji wa Madini katika baadhi ya maeneo, Uvuvi kwa wananchi wanaoishi karibu na mito, maziwa na bahari. Kundi hili kubwa linapaswa kupelekewa na kuboreshewa huduma mbalimbali za kijamii ili kuimarisha mfumo kazi kwa ajili ya kujenga Uchumi nchi yetu.
Kila awamu ya uongozi wa nchi yetu imefanya jitihada kubwa sana kupeleka maendeleo vijijini.
Awamu ya tano chini ya Hayati Rais Dkt. John Magufuli ilisambaza umeme katika vijiji vingi sana, miradi mikubwa ya maji vijijini, ujenzi wa barabara, na kuanza utekelezaji wa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari, hatua ambayo imekuwa na tija kubwa kwa maendeleo vijijini.
Sitaki kusema kwamba maendeleo katika miji na majiji hapa nchini hayahitaji kuboreshwa zaidi pamoja na hupatikanaji wa huduma za kijamii ikilinganishwa na vijijini, bado kuna umuhimu huo kama inavyofanya serikali ya awamu ya sita kupeleka maendeleo mijini na vijijini.
Jumatano ya Desemba 8, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alihutubia Taifa kwa njia ya televisheni na kueleza mafanikio na changamoto katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo, ufugaji na uvuvi katika kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika.
Kuhusu ukuaji wa sekta hizo hapa nchini alisisitiza mageuzi makubwa kufanyika ili ukuaji wa sekta hizo kwenda sambamba na kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia
“Tunapoangalia mbele tunakwenda kuandaa dira ya miaka 25 ijayo ambayo itatutoa mwaka 2025 hadi mwaka 2050 itaelekeza kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kutoa kipaumbele kwa sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja kama sekta ya kilimo,” anaeleza Rais Samia.
Baada ya kutimiza mwaka mmoja madarakani machi, 2022, Rais Samia alieleza utekelezaji wa vipaumbele vyake ambavyo mara kwa mara amekuwa akitilia mkazo hasa Ufugaji, Uvuvi na Kilimo cha Umwagiliaji.
“Umwagiliaji ni mambo mawili kwanza tunachukua hatua ya kurekebisha mfumo wa Tume ya umwagiliaji yenyewe, tunaanza kule lakini pili tunaongeza bajeti ya kilimo, mkazo mkubwa tumeweka kwenye kilimo cha umwagiliaji kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi na kiuchumi,” anasema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kutoa ruzuku katika mazao ya kimkakati ambayo ni korosho, pamba na kahawa na tayari imeboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta ya kilimo hapa nchini.
Aprili 4, 2022, serikali ilizindua kauli mbiu ya “Kilimo ni Biashara” ambayo inawapa hamasa wakulima na wadau wengine kuondoa dhana ya unyonge kwa kuwa zipo fursa nyingi za kuondokana na umaskini kupitia Sekta ya kilimo.
“Tunaelekea kwenye kilimo cha kisasa, niwaambie vijana waingie huko ili kwenda kupata fedha za halali lazima tufanye mapinduzi makubwa ambayo yanatupa uhakika wa kulisha watu wanaongezeka duniani na kukuza soko la biashara,” anabainisha Rais Samia.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba anaeleza mikakati ya serikali kukuza soko la ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti ya Wizara hiyo na kwamba hiyo ni mikakati endelevu. “Ili kupunguza umaskini kwa watanzania, serikali inalenga kutengeza ajira kwa vijana na wanawake zaidi ya milioni tatu katika sekta ya kilimo ifikapo mwaka 2025,” alisema Dkt. Mwigulu.
Mageuzi makubwa ya kilimo, mifugo na Uvuvi yalitajwa pia na Rais Samia katika kilele cha maadhimisha ya siku ya wakulima Nane Nane yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Mbeya mwaka huu.
Rais Samia aliwataka Mawaziri wanaohusika na Taasisi mbalimbali za serikali kutekeleza mikakati hiyo na kusimamia mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi kwa kufanya Sheria, kuanzisha viwanda vya mbolea, kuimarisha kilimo cha umwagiliaji na cha bustani ili kutimiza azma ya kukuza kilimo kwa asilimia 10.
Waziri wa kilimo Hussein Bashe alisema zaidi ya Shs. bilioni 200 zinatarajiwa kutumika kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima katika msimu huu wa kilimo na kufanya matumizi ya mbolea kufikia tani 650,000.
Kwenye Wizara ya mifugo na Uvuvi Waziri Abdallah Ulega anaeleza kwamba kazi ya magenzi inaendelea vizuri tayari wamenunua boti 160 za kisasa maalumu za kufugia samaki aina ya sato na tayari vijana na kina mama wameshakabidhiwa mkoani Mwanza kuimarisha Uzalishaji wao.
Serikali pia imetumia fedha za Uviko-19 kwa kujenga Zahanati, Hospital na vyumba vya madarasa sehemu mbalimbali hapa nchini na kuelekeza nguvu katika maeneo ya vijijini lengo likiwa ni kuinua maisha ya wananchi waishio vijijini.
Mradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR) ambao umepita katika vijiji vingi hapa nchini, Mradi huo umetoa ajira kwa wananchi wa maeneo hayo na utatoa fursa mbalimbali za kiuchumi pindi utakapo kamilika.
Kwa nyakati tofauti serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika maeneo ya vijijini na kuimarisha huduma ya mawasiliano kwa kujenga minara mingi ya simu katika maeneo hayo.
Mei 13, 2023 Rais Samia alitangaza mapinduzi makubwa katika teknolojia ya mawasiliano ambayo wananchi wa maeneo ya vijijini watanufaika na huduma bora za mawasiliano ya simu, Matibabu, Taarifa za masoko kwa wakulima, Usalama na elimu kwa kutumia simu za kisasa na njia ya mtandao.
Mageuzi hayo makubwa yalitangazwa jijini Dodoma baada ya serikali kusaini mikataba ya miradi miwili ya ujenzi wa minara 758 ya simu katika kata 713 na mradi wa kuongeza nguvu ya minara 304 katika maeneo ya vijijini kwa mikoa yote ya Tanzania Bara.
Serikali tayari kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote (UCSAF) imeshaingia makubaliano na kampuni za Simu kufikisha huduma za mawasiliano katika kata 1380 ambapo wakazi zaidi ya milioni 15.7 watanufaika hususani maeneo ya vijijini.
Rais Samia alisema hatua hiyo itaimarisha upatikanaji wa mawasiliano vijijini na kuondoa tabaka baina ya waishio vijijini na maeneo ya mijini na kwamba mawasiliano hayo yatakuza uchumi na biashara vijijini pia upatikanaji wa masoko.
“Kadhia ya ukosefu wa mawasiliano inakwenda kuondoka kwa wakulima na wananchi wetu vijijini, atakapoweza kulima na kuvuna, vizuri anakwenda kupata soko la uhakika kwa sababu taarifa za soko atakuwa nazo kiganjani mwake, kwa hiyo tunakwenda kubadilisha teknolojia vijijini”, anasisitiza Rais Samia.
Jumatatu ya Novemba 6, 2023 Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo aliliambia Bunge kwamba kwa kuwa asilimia 61 ya nguvu kazi iko katika sekta ya kilimo, alipendekeza mipango ijayo ya maendeleo iweka mkazo maalumu kuhakikisha uchumi wa vijijini unakuwa Sehemu muhimu ya uchumi wa Taifa.
Katika kuboresha na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii vijijini alipendekeza kuchukua hatua saba ikiwemo kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kuweka mazingira maalumu katika kuvutia ujenzi wa viwanda vidogo vijijini.
Alisema hatua nyingine ni serikali kutumia sera za kifedha na kikodi kuvutia wawekezaji katika maeneo ya vijijini, kuendelea kupanua na kuboresha miundombinu ya huduma za afya, elimu, maji na umeme pamoja na kuhakikisha angalau asilimia 30 ya wananchi vijijini wanakuwa na bima ya afya ifikapo mwaka 2025.
Profesa Kitila alieleza hatua nyingine kuwa ni kuweka mkazo wa pekee katika kuimarisha ubora wa elimu kuzingatia umuhimu wa digitali katika kuleta mapinduzi ya uchumi vijijini na kupitia upya Sera za fedha sheria na kanuni zinazosimamia mikopo kwa lengo la kuzisukuma Taasisi za kifedha kuelekeza mikopo katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo.