Na Florian Kaijage
BBC Swahili, Dar es Salaam
ASKOFU wa Jimbo Katoliki Geita nchini Tanzania, Flavian Kassala amesema hayuko tayari kubariki ndoa ya jinsia moja kwani ni kinyume na maagano ya Mungu ya kutaka binadamu wakazaliane na kuendeleza kazi ya uumbaji.
Akihubiri katika misa ya kitaifa ya Krisimasi iliyorushwa mubashara na Televisheni ya Taifa (TBC), amesema kubariki mapenzi ya jinsia moja ni kwenda kinyume na maandiko ya Mungu yanayotaka wanadamu wakazaliane na kuendeleza vizazi.
“Tumeingia kati hali ambayo tunabomoa hata njia za ujio wa watoto, mahusiano ya binadamu ambayo yanaondoa kabisa nafasi ya Mungu kuendeleza kazi ya uumbaji, wengine munayaita ndoa za jinsia, hakuna ndoa ya jinsia moja, ndoa ni moja tu, hata katika maangaiko yake ni uhusiano wa mke na mume, binadamu na si binadamu na mnyama wa kiume au wakike na kama tumeshindwa kuyatenda hayo kwa wanyama imegeuka sasa kati yetu na kupiga kelele jambo hili lihalalishwe”.
Amesema binadamu anakataa uumbaji wa Mungu na kufanya mambo yaliyokatazwa huku wakitaka na kanisa liyabariki jambo ambalo amesema yeye hawezi kulifanya kamwe.
“Katika uchafu huo Sasa tunaomba tupewe na baraka, uje nikubariki katika hilo ambalo halina matumaini yoyote. Ni bora uniletee jiwe nitabariki ukajenge nyumba imara kuliko hali hiyo ambayo tunafikia sasa na kupigania na kuona ni haki” amesema Askofu Kassala.
Jumatatu Desemba 18, Vatican ilitoa waraka ulioidhinishwa na Papa Francis ukifafanua maana ya baraka, aina zake na utekelezaji.
Pia waraka huo uliruhusu makasisi wa Kanisa Katoliki kuwabariki wapenzi wa jinsi moja.
Wataalamu wanasema hati iliyoidhinishwa na Papa Francis na iliyotolewa tarehe 18 Disemba haionyeshi dalili zozote kwamba Kanisa linakusudia kuchukua hatua zaidi za kukubali ndoa za watu wa jinsia moja.
Hata hivyo Vatican ilisema kuwa kuwabariki wapenzi hao wa jinsi moja haimaanishi kuwa ni kubariki ndoa za jinsi moja bali baraka hiyo ni kwa watu wenyewe binafsi wenye uhitaji bila kujali hali zao za kiroho na kwamba ni jambo jepesi lislozingatia uzito wa baraka za kisakramenti au kiliturjia.
Vatican ilieleza pia kupitia waraka huo kuwa msimamo wa Kanisa Katoliki kuhusu ndoa haujabadilika na kwamba ndoa ni muunganko kati ya mwanamume na mwanamke.
Hata hivyo, waraka huo ulipokewa kwa mitazamo tofauti hususan Barani Afrika, ambako mabaraza ya maaskofu Katoliki katika nchi za Nigeria, Zambia, Malawi na Madagascar yalitoa nyaraka za kimaandishi kufafanua kwa waumini wao.
Mfano baraza la maaskofu la Zambia lilisema waraka wa Vatican kuwabariki wapenzi wa jinsi moja halitekelezeki nchini huo kwani, linakiuka mafundisho ya dini, mila desturi na sheria za nchi hiyo.
Kadhalika Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam nchini Tanzania, Yuda Theddeus Ruwa’ichi alisema hawezi kuwabariki watu wawili wa jinsi moja wanaokwenda kwake.
Jumapili Desemba 24 Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Nairobi, Kenya Philip Wanyolo alitoa waraka unaokubaliana na msimamo wa Kanisa juu ya ndoa.
Lakini alipiga marufuku aina yoyote ya baraka ya makasisi wa jimbo hilo kwa uhusiano wowote usio rasmi au wapenzi wa jinsi moja, kwani kufanya hivyo ni kwenda kinyume na neno la Mungu, mafundisho ya kanisa, utamaduni wa kiafrika sheria za mataifa na kwamba ni kashfa dhidi ya imani.
Katika waraka wa Desemba 18, 2023 inaelezwa kuwa Papa Francis aliwaruhusu mapadre kuwabariki wapenzi wa jinsi moja, yakiwa ni maendeleo makubwa kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsi moja na mahusiano mengine ya kijinsia wanaofahamika kama LGBT katika Kanisa Katoliki la Roma.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki la Roma akasema makasisi wanapaswa kuruhusiwa kuwabariki wapenzi wa jinsi moja na wanandoa “isiyo ya kawaida”, kwa misingi ya hali fulani.
Lakini Vatican ilisema baraka hazipaswi kuwa sehemu ya taratibu za kawaida za Kanisa au zinazohusiana na miungano ya kiraia au harusi.
Iliongeza kuwa inaendelea kuiona ndoa kuwa kati ya mwanamume na mwanamke.
Papa Francis aliidhinisha waraka uliotolewa na Vatican kutangaza mabadiliko hayo siku ya Jumatatu.
Vatican ilisema inapaswa kuwa ishara kwamba “Mungu anawakaribisha wote”, lakini hati hiyo inasema Makasisi lazima waamue kwa kuzingatia uhalisia wa kila tukio.
Akitambulisha andiko hilo, Kardinali Víctor Manuel Fernández, ambaye ni msimamizi wa Kanisa, alisema kwamba tamko jipya limebakia kuwa “imara kwenye fundisho la kimapokeo la Kanisa kuhusu ndoa”.
Lakini aliongeza kuwa kwa kuzingatia “maono ya kichungaji” ya Papa” ya “kupanua” ombi la Kanisa Katoliki, miongozo mipya inawaruhusu mapadre kubariki uhusiano ambao bado unachukuliwa kuwa wa dhambi.
Watu wanaopokea baraka “haifai kuhitajika kuwa na ukamilifu wa kimaadili wa awali”, kulingana na tamko hilo.
Katika Kanisa Katoliki, baraka ni maombi au ombi, ambalo kwa kawaida hutolewa na mhudumu, akimwomba Mungu ambariki mtu au watu wanaobarikiwa.
Kardinali Fernández alisisitiza kwamba msimamo huo mpya hauhalalishi hadhi ya wapenzi wa jinsia moja mbele ya Kanisa Katoliki.
Tamko hilo linawakilisha urejeshaji wa sauti kutoka kwa Kanisa Katoliki, ingawa sio mabadiliko ya msimamo.
Mnamo 2021, Papa alisema makasisi hawawezi kubariki ndoa za watu wa jinsia moja kwa sababu Mungu hawezi “kubariki dhambi”.
Mnamo mwezi Oktoba Papa Francis alikuwa amependekeza kwamba alikuwa wazi kuhusu Kanisa kuwabariki wapenzi wa jinsi moja.
Maaskofu katika nchi fulani hapo awali wameruhusu mapadre kuwabariki wapenzi wa jinsi moja, ingawa msimamo wa mamlaka ya Kanisa haikufahamika wazi.