Na Kija Elias, Kilimanjaro
WANANCHI wa Kata ya Arusha Chini, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, wamefurahia kuimarika kwa huduma za afya katika Hospitali ya TPC, wakisema hali hiyo siyo tu imewapunguzia gharama za matibabu bali pia imewaepusha kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Mkazi wa Kijiji cha Mserekia, Ramadhan Abdully, anasema moja ya matunda ya wawekezaji wanaowekeza katika eneo lolote lile ni kuonyesha ushirikiano na wenyeji husika, katika kusaidia shughuli za kijamii kama wanavyofanya Kiwanda cha sukari TPC.
Anasema kuwa TPC imekuwa na mchango makubwa sana kwetu sisi Wananchi wa vijiji vinavyozunguka kiwanda hiki na endepo kisingekuwepo kiwanda hiki nakuhakikishia maendeeleo haya unayaona sasa yasingekuwepo.
Mariam Mmari ni mama wa watoto watatu, ambaye anasema kuanza kufanya kazi kwa huduma za upasuaji na mionzi katika hospitali hiyo ni ukombozi kwa akina mama wajawazito wanaoishi karibu
Mariam anayejishughulisha na kilimo cha mpunga anasema: “Zamani walikuwa wanahangaika, mwanamke anapobeba mimba alikuwa akilazimika kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi, sasa hivi hali ni nzuri, watu wanahudumiwa hapa karibu. hawahangaiki tena.”
Mwananchi mwingine, Renatus Kitomari, anasema huduma hizi zimeleta tabasamu kwa wanawake na wanaume wa Kata ya Arusha Chini “Tuna furaha kwa sababu huduma ziko karibu, ukipata tatizo unakimbia haraka haraka,” anaeleza baba huyo wa watoto wanne. “Ukiona kama wameshindwa hapa, unaona gari inakuja kukuchukua na kukupeleka KCMC.”
Mkazi mwingine wa Kijiji cha Loondoto, Asia Msangi, anasema “Tunakishukuru sana Kiwanda cha TPC kwa kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuleta vifaa tiba vya kisasa katika hospitali hii.
“Sehemu yoyote yenye rasilimali kitu cha kwanza wanaotakiwa kunufaika na rasilimali hiyo ni Wananchi wa eneo husika kwa kuwa ndiyo walioweza kuitunza vyema mali hiyo,” anasema Msangi.
Akizungumza baada ya kuzindua majengo mapya matatu ya huduma kwa wateja katika hospitali ya TPC Mkuu wa Wilaya ya Kisare Makori, amesema Serikali inathamini mchango unaotolewa na Sekta binafsi katika kuhudumia Wananchi na masuala ya mengine ya kijamii na kupongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Kiwanda Kiwanda cha Sukari TPC kwenye nyanja za huduma za afya kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.
Makori anasema Serikali kwa kutambua umuhimu wa afya katika mwaka wa fedha 2023-2024 imetoa kiasi cha Shs. bilioni 1.8 kwa ajili ya upanuzi na ukarabati wa hospitali ya Wilaya katika Kata ya Mabigini.
“Serikali pia imetoa Shs. milioni 870 kwaajili ya uboreshaji wa Huduma za afya Kituo cha Afya Uru Kusini, Shs. milioni 500 kituo cha Kahe na Shs. milioni 500 kituo cha afya Marangu.”
Aidha, anasema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha huduma mbalimbali za kijamii nchini, zikiwemo za afya, hivyo amewataka wananchi waendelee kuipa ushirikiano.
Awali Ofisa Utawala wa Kiwanda cha TPC Jafari Ally, anasema Hospitali ya TPC ilianza mwaka 1945 na kipindi chote hiki imekuwa ikihudumia wafanyakazi na Wananchi jirani na kiwanda kwa kutambua uhitaji wa huduma za afya na ongezeko la wakazi katika eneo hili ambao sasa wamefikia 95,000 wameamua kuipanua hospitali hiyo ambayo kwa sasa itakuwa na hadhi ya nyota nne.
Anasema kwa miaka mitano iliyopita TPC imetumia zaidi ya Shs. bilioni 1.2 kujenga majengo mapya, kuboresha yaliyopo na kununua vifaa tiba kwa lengo la kuendelea kutoa Huduma kwa jamii inayozunguka eneo la kiwanda hicho.
“TPC imeamua kupanua hospitali hiyo kwa awamu na kwa miaka mitano iliyopita tumetumia zaidi ya Sh bilioni 1.2 kujenga majengo mapya, kuboresha yaliyopo na kununua vifaa tiba, tumejenga wodi ya daraja la kwanza, wodi maalumu kwa magonjwa ambukizi, jengo la huduma ya mama na mtoto RCH kuboresha wodi zote za akina mama, wanaume na watoto,” anasema Ally.
Pia anasema wamenununa vifaa muhimu vya kutolea Huduma ikiwemo gari la wagonjwa, mashine za theatre, mashine za mionzi, utra sound, kiti cha huduma ya meno na ventilator na kuongeza wataalamu tiba wabobevu.
Aidha, anasema TPC imeanzisha huduma za kibingwa kwa kuajiri madaktari bingwa wawili akiwemo daktari wa magonjwa ya aika mama na daktari bingwa wa mifupa na kwamba huduma hiyo itatolewa hospitalini hapo hasa ikizingatiwa tayari jengo yameshakamilika.
Pia Ally anasema kiwanda cha TPC kimefadhili ujenzi wa zahanati tano, katika vijiji vilivyo mbali na TPC, vijiji hivyo ni pamoja na kijiji cha Mserekia, Loondoto, Mawala, Kirungu na Chemchem, sambamba na kuiboresha zahanati ya Mikocheni.
Meneja wa Hospitali ya TPC Lazaro Urio, amesema kuwa hospitali hiyo imejiunga na huduma za bima za afya, pamoja na kutoa huduma ya upasuaji ambapo huduma zote muhimu zinapatikana muda wote kutokana na hospitali hiyo kuwa na madaktari bingwa jambo ambalo limerahisisha wagonjwa kupata huduma karibu zaidi na kwa uharaka.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Arusha Chini, Leonard Waziri, ameushukuru uongozi wa Kiwanda cha TPC kwa kuendelea kuwekeza zaidi huduma za kijamii kwani Wananchi wamefurahia kuimarika kwa huduma za afya zinazotolewa katika TPC, wakisema hali hiyo siyo tu imewapunguzia gharama za matibabu bali pia imewaepusha kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Anasema takwimu za Sensa za Watu na Makazi ziliyofanyika mwaka 2022 zinaonesha Kata ya Arusha Chini ina wakazi 13,977 huku kaya zikiwa 3,735, wananchi hao walikuwa wakipata adha kubwa ya huduma za afya, kuboreshwa kwa hospitali hiyo kutasaidia Wananchi wa kata ya Arusha Chini kupata huduma bora na karibu badala ya kwenda hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mawenzi.
“Wananchi wa kata hii pamoja na walioko kata jirani wamekuwa wakinufaika sana na huduma mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji umeme na barabara kutoka kiwanda hiki cha Sukari TPC,” anasema Diwani Waziri.