Arsenal, Chelsea zapiga watu ‘mkono’

WASHINGTON DC, Marekani

TIMU za Arsenal na Chelsea, zimeibuka na ushindi wa mabao 5-0 kila moja katika mechi zao za kirafiki kujiandaa na msimu mpya.

Arsenal ikiwa jijini hapa, iliitandika MLS All-Stars iliyokuwa ikinolewa na Kocha, Wayne Rooney mabao hayo huku kiungo wao ghali, Declan Rice akicheza kwa mara ya kwanza ndani ya kikosi hicho.

Kiungo huyo, 24, alikamilisha usajili wake wa pauni milioni 105 akitokea West Ham Jumamosi na siku nne baadaye alianza safari umbali wa maili 3,660 kuelekea uwanjani Emirates.

Rice aliingia kipindi cha pili wakati kikosi hicho cha Rooney kikipata wakati mgumu kwenye mchezo huo kupata matokeo.

Mabao ya Arsenal katika mchezo huo, yalifungwa na Gabriel Jesus, Leandro Trossard, Jorginho kwa mkwaju wa penalti, Gabriel Martinelli na Kai Havertz akifunga bao lake la kwanza tangu asajiliwe akitokea Chelsea.

Kabla ya mchezo huo, Mkurugenzi wa Klabu ya Arsenal, Josh Kroenke, alishangiliwa na umati wa mashabiki waliokuwa uwanjani Audi Field baada ya kutambulishwa na hivyo hivyo mashabiki hao walifanya kwa Rooney alipotambulishwa.

Katika mchezo mwingine wa kirafiki, Chelsea ilitandika Wrexham mabao 5-0 huku kinda wao, Ian Maatsen akifunga mabao mawili.

Mabao mengine yalifungwa na Conor Gallagher, Christopher Nkunku na Ben Chilwell.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *