
Na Mwandishi Wetu, Lindi
MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye amesema mtu anayehoji utu wa Mgombea Urais wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassan atakuwa na dhamira ya kuwakoroga Watanzania na kuwaomba wasikorogeke.
Akiongea katika mkutano wa kampeni wa mgombea huyo wa CCM alisema kauli mbiu ya Kazi na Utu, Tunasonga Mbele imetokana wa utenda kazi wa Rais Samia ambaye ndani ya miaka minne ya urais wake imekuwa kielelezo cha kiongozi mwenye utu.
Akifafanua Nape amesema katika kipindi cha miaka minne cha serikali ya awamu ya sita imeajiri zaidi ya watu 155,000 kwenye sekta mbalimbali katika wakati ambao ajira ilikuwa imesimamishwa serikali kwa muda kushughulikia wafanyakazi hewa na kwa takribani miaka sita wafanyakazi hawakuwa wamepanda madaraja wala kuongezewa mishahara, lakini utu wa Samia umefanya alipoingia madarakani, ayatekeleze hayo.
“Anayehoji utu wako (Samia), anajitoa ufahamu au ameamua kuwakoroga Watanzania. Nataka nikwambie, sisi wana Mtama wajanja, hatukorogeki,” amesema.
Akifafanua zaidi amesema utu wa Rais Samia haukuishia hapo, uliendelea kujipambanua zaidi aliporuhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa iliyokuwa imefungiwa kwa zaidi ya miaka sita.
“Kwa mara ya kwanza, Mama huyu akawaambia andamaneni nitaleta Ambulance, nawalinda, mkimaliza nendeni nyumbani mkalale, nani kama Samia,” amesema Nape.
Akihutubia mkutano huo wa kampeni Rais Samia amesema katika miaka mitano ijayo, atahakikisha huduma za kijamii zinapatikana ikiwemo maji na umeme na kuahidi kuendelea kuusambaza katika vitongoji, pamoja na kugawa majiko yanayotumia nishati kidogo ili kuepusha matumizi ya kuni na mkaa.
Amesema atahamasisha kilimo cha mazao ya chakula na biashara ili yazalishwe kwa wingi kwa kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo. Aliwahamasisha wakulima kuendelea na kilimo kwa kuwa Tanzania ina uwezo wa kulisha nchi tisa ambazo zote zikipatwa tatizo zinaikimbilia.
Akiwa wilayani Ruangwa Rais Samia amemtaja Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa sehemu ya mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kwa kuwa ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali.
Alieleza Ruangwa imetoa msaidizi mzuri wa Serikali aliyeitumikia nafasi ya uwaziri mkuu kwa miaka 10 na kwamba anamshukuru Majaliwa kwa ushirikiano, kujituma na uzalendo wakati wote walipofanya kazi pamoja.
Samia amekwenda mbali zaidi na kueleza, mazuri yanayoelezwa na kuonekana sasa katika Jimbo la Ruangwa ni matokeo ya juhudi, msukumo na nguvu ya Majaliwa alipokuwa mbunge.
“Katika kuuthamini na kuutambua mchango wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameacha kuwa waziri mkuu ameacha kuwa mbunge, anaendelea kuwa msaidizi makini na muhimu katika Serikali yetu, hiyo ndiyo ahadi yangu kwenu,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo Ruangwa, Majaliwa amesema wananchi wa eneo hilo wana sababu lukuki za kumpigia kura Samia katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Maboresho ya wilaya hiyo kutoka kuwa na changamoto nyingi za huduma za jamii hadi kusalia chache ni miongoni mwa sababu zitakazowafanya wananchi wamchague Samia.
Amezitaja sababu nyingine ni maboresho ya miundombinu hasa ya barabara na miradi ya kimkakati ikiwemo mpango wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR).
“Reli hii utaitekeleza wewe tunakuachaje, Oktoba 29, katika Uchaguzi Mkuu? Haya yanatupa sababu Wana-Lindi kukupigia kura za ndiyo siku ya uchaguzi. Mimi niko na yeye ndiye msaidizi wake ofisini kwake,” amesema Majaliwa.
Suluhu Hassan amesema ingawa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, hatakua na wadhifa alionao sasa, Serikali yake katika miaka mitano ijayo, itaendelea kumtumia kama msaidizi muhimu serikalini.
Sambamba na Majaliwa, Rais Samia amemtaja Mgombea ubunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye kuwa kijana hodari, mchapakazi mzuri, anayeijua siasa na aghalabu anamtambua kama kamanda.
Kauli hizo za Samia kwa wanasiasa hao ni kama jawabu kwa wanaodai Majaliwa na Nape si miongoni mwa watu wenye uhusiano mzuri na mgombea huyo wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Minong’ono hiyo iliibuka baada ya Majaliwa kutangaza mpango wa kutogombea tena ubunge wa Ruangwa. Kwa upande wa Nape ilitokana na hatua ya kuondolewa katika wadhifa wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Julai 21, mwaka jana.
Mgombeea huyo wa urais kwa tiketi ya CCM, ametoa kauli hizo kwa nyakati tofauti alipokuwa katika mikutano ya kampeni katika majimbo ya Ruangwa na Mtama mkoani Lindi, iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi.



