Amsha amsha Betika Mbeya Tulia Marathon kuanzia Dar J’mosi

Na Mwandishi Wetu

AMSHA amsha ya mbio za Betika Mbeya Tulia Marathoni msimu huu, itaanzia Jumamosi jijini Dar es Salaam.

Mbio hizo zinazoshirikisha nyota wa riadha nchini zitafanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya ikishirikisha mbio fupi za uwanjani Mei 9 na mbio ndefu za marathoni Mei 10.

Akizungumza wakati wa kukabidhiwa jezi itakayotumika msimu huu kutoka kwa washirika wa mbio hiyo, Times FM na Kampuni ya Michezo ya Kubashiri ya Betika, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema mkoa huo utawagharamia wakimbia 200 nauli ya kwenda Mbeya kushiriki mbio hizo.

“Ili kuhamasisha hilo, Jumamosi tutafanya amsha amsha kwa watu wa Dar es Salaam kujiweka fiti kushiriki mbio hizo,” amesema Chalamila na kuongeza;

“Amsha amsha yetu itaanzia Aga Khan kwenda fukwe ya Coco kuanzia saa 12 asubuhi”.

Amesema watu 200 watakaofika wa kwanza kwenye amsha amsha watagharamiwa nauli ya kwenda Mbeya kuchuana kwenye mbio hiyo msimu huu.

“Msimu huu, Dar es Salaam tunataka tukathibitishe ubora wetu kwenye riadha, huwa tunasema watu wa Dar hatuna nguvu, msimu huu kwenye Betika Mbeya Tulia Marathoni tunakwenda kuthibitisha ubora wetu,” amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Times FM, Rehure Nyaulawa, amesema wao kama moja ya wawezeshaji wa mbio hizo wamejipanga kuhakiisha msimu huu inafanyika kwa ubora zaidi.

“Kama mjuavyo, Times Radio maudhui yake kwa asilimia kubwa ni ya kimichezo, tunaona fahari kuwa washirika wa Tulia Trust Foundation katika kutangaza hizi mbio ambazo mlezi wake ni Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson,” amesema.

Pia Ofisa Habari wa Betika, Rugambwa Juvenalius, amesema msimu huu kampuni hiyo ambayo ni mdhamini imejipanga kuendeleza ubora wa mbio hizo ili izidi kuwa kubwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *