Na Asha Kigundula
MTANZANIA Alice Gyunda ni miongoni mwa washiriki 20 kutoka nchi mbalimbali za Afrika waliofanikiwa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha taji la Miss /Mrs Afrika shindano ambalo linalifanyika nchini Uingereza.
Akizungumza na gazeti hili hili kuhusu undani wa shindano hilo, Alice amesema amevutiwa kujiunga kwenye shindano hilo ambalo kuna vitu tofauti tofauti anatarajia kuvifanya.
Amesema malengo yake kama watanzania watampigia kura na kushinda ana mpango wa kuanzisha vituo vya kuibua vipaji kwa wasanii wa sanaa ya muziki kila mkoa.
Amesema kupitia vituo hivyo vya kuibua vipaji kwa watoto pia vitakuwa na mkakati endelevu wa kutunza wasanii watakaopatikana katika vituo hivyo kwa kuwawezesha kupata taalum ya sanaa ya muziki.
Aidha Alice akafika mbali zaidi kwa kuainisha mikakati aliyonayo katika kuwaunganisha vipaji vitakavyopatikana hapa nchini na kuunganisha na taasisi nyingine za nchini uingereza ambazo zinaibua vipaji vya sanaa mbalimbali ikiwamo ya muziki.
Aidha anasema uanzishwaji wa vituo vya uibuaji vipaji vitakavyoanzishwa vitakamilika katika sekta zote za uwepo wa studio za kisasa kwa ajili ya kurekodi nyimbo ambapo pia kwa wasanii watakaofanya vizuri wataunganishwa kufanya muziki wa pamoja na wasanii wakubwa wa Tanzania pamona na w Afrika na Ulaya.
Amesema lengo la kuanzisha vituo hivyo vya kuibua vipaji ni kutaka kuandaa wasanii wengi wakubwa wa muziki wa Bongofleva, Hiphop, Singeli na Reggae.
Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kuandaa wasanii wengi wazuri wakati wale wakongwe kama akina Diamond, Alikiba na Harmonize na wengine watakapokuwa wamemaliza zama zao.
Shindano la Miss/Mrs. Afrika UK ni shindano linaloshirikisha waafrika wanaishi nchini Uingereza ambao walifanikiwa kuingia baada ya kukidhi vigezo vya kuingia kwenye shindano hilo ambalo linaandaliwa na taasisi ya Africauk Pageants ya nchini Afrika Kusini.
Tayari awamu ya kwanza ya mchujo imepita na kupatikana warembo 20 watakaoingia kwenye tano bora hadi kupatikana mshindi wa kwanza hadi wa tatu na anaomba kura yako kwani amesema ushindi wake ni ushindi wa watanzania.
Amesema ushindi wa shindano hilo ni namna mshirika anavyopigiwa kura kupitia mtandao wa https//afrikaukpageants. co. uk/poll/mrs-missafrica-finalist-2023.
Hata hivyo bado nguvu ya watanzania katika kumpigia kura mrembo huyo imekuwa ni ndogo tofauti na namna ya ushiriki wa taifa jirani la Uganda ambapo wanajitokeza kwa wingi kumpigia kura mshiriki wao.
Kutokana na changamoto hiyo, mshiriki Alice Gyunda amewaomba watanzania kutoka nchi mbali mbali kushiriki kumuunga mkono kwa kumpigia kura nyingi za ndiyo kupitia link ilianishwa hapo juu ambapo mwisho wa kupiga kura ni Septemba 10.
Anasema ushindi wake ni fursa kwa watanzania ambapo kwa mujibu wa zawadi zilizoanishwa kwenye shindano hilo pamoja na mshindi atakayetwaa taji hilo atapata fursa ya kuandika andiko la namna atakavyosaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika nchi yake ya uraia.
Hadi sasa ni asilimia sita ya upigaji kura wa watanzania katika shindano hilo huku mshiriki wa Uganda akiongoza kwa asilimia 39 na kuwaacha mbali washiriki wengine akiwamo Mtanzania alice Gyunda
Mtanzania huyo ametoa msada wa vitu mbalimbali kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika Halmashauri ya Mkuranga ikiwamo unga, sabuni, mchele, mafuta ya kula ili kusaidia makundi hayo.
Mrembo Alice taaluma yake ni mwalimu ambapo kabla ya kwenda kuishi ughaibuni akiwa nchini Tanzania amewahi kufundisha katika Shule ya Msingi Kawe na Osterybay.
Pia mshiriki huyo ana kipaji cha usanii wa sanaa ya nyimbo zenye maudhui ya uelimishaji.