LONDON, England
NYOTA namba moja duniani katika tenisi, Mhispania, Carlos Alcaraz, ametinga nusu fainali ya michuano ya Wimbledon kwa mara ya kwanza na ataumana na Mrusi, Daniil Medvedev ambaye ni wa tatu kwa ubora.
Alcaraz alimtandika Holger Rune ambaye ni raia wa Denmark kwa seti 7-6 (7-3) 6-4 6-4 katika robo fainali.
Chris Eubanks ambaye hakupewa nafasi katika michuano hiyo, ndoto zake zilizimwa kwa kufungwa na Medvedev, 27 katika mchezo uliokuwa na seti tano za moto.
Medvedev ambaye hakuwahi kuvuka hatia ya 16 Bora hapo awali, alimfunga Mmarekani huyo kwa seti 6-4 1-6 4-6 7-6 (7-4) 6-1.
Kwa sasa Alcaraz na Medvedev ambao walitwaa mataji katika uwanja wa udongo kwenye michuano ya US Open, kila mmoja atapambana kutinga fainali yake ya kwanza kwenye uwanja wa majani wakati watakapoumana leo.
Katika nusu fainali nyingine, Mserbia Novak Djokovic ambaye kwa ubora ni wa pili duniani, atawania kuweka rekodi kwa upande wa wanaume mchezaji mmoja mmoja kutwaa taji lake la nane atakapoumana na Jannik Sinner.
Kwa upande wa wanawake, bingwa mtetezi wa michuano hiyo, Elena Rybakina, alivuliwa ubingwa katika robo fainali kwa kufungwa na Ons Jabeur akilipa kisasi cha mwaka jana.
Jabeur ambaye ni wa sita kwa ubora upande wa wanawake, alishinda kwa seti 6-7 (5-7) 6-4 6-1.
Jabeur ataumana na Aryna Sabalenka katika nusu fainali itakayopigwa Jumanne baada ya kumtandika Madison Keys.