Akiba ya gesi asilia ni utajiri mkubwa

Na Salha Mohamed

SEKTA ya mafuta na gesi asilia iligundulika kwa mara ya kwanza hapa nchini mwaka 1974 katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi, ugunduzi mwingine umefanyika Mkoa wa Mtwara mwaka 1982 eneo la Mnazibay.

Jumla ya gesi asilia iliyogundulika nchi kavu na baharini inafikia takriban futi za ujazo trilioni 55.08 hadi kufikia Machi 2015.

Mafuta na gesi asilia yanaweza kupatikana katika miamba tabaka (sedimentary rocks) ndiyo yenye uwezo wa kutoa mafuta au gesi ambapo hapa Tanzania maeneo hayo ni ya Pwani, Mtwara, na Lindi na mabonde ya nchi kavu. Utafiti unaonesha kuwa karibu nusu ya Tanzania kuna uwezekano wa kupatikana mafuta na gesi.

Licha ya changamoto zilizopo katika sekta ya mafuta na gesi kama gharama kubwa ya kuchimba visima wakati wa utafiti, serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ya kuiwezesha Sekta Mafuta na Gesi iweze kuchangia ipasavyo katika maendeleo ya nchi.

Gesi iliyoko kwenye kina kirefu cha bahari kusini mwa Tanzania ipo katika vitalu vilivyopo zaidi ya kilomita 100 kutoka kwenye ufukwe wa bahari, na kwenye kina cha bahari chenye urefu wa mita 2,500 kufikia kwenye sakafu ya bahari na mita 2,500 chini ya sakafu ya bahari. Umbali kati ya vitalu unaweza kuwa zaidi ya kilomita 100.

Teknolojia ya kiwango cha juu ya utafutaji gesi inatumika kutokana na mradi kuwa katika kina kirefu, umbali mrefu kutoka ufukweni na hali ya ardhi na miamba ilivyokaa chini ya bahari.

Teknolojia hiyo pia hutoa fursa ya kipekee ya kujenga Uwezo wa kiufundi kwa watoa huduma kwenye Sekta ya gesi na ndani ya TPDC.

Ukubwa wa ugunduzi baharini, umbali mrefu kutoka ufukwe wa Tanzania na gharama za kuendeleza vitalu vya gesi katika kina kirefu ili kuleta gesi ufukweni, vinahitaji uwepo wa soko lililo tayari litakalo halalisha uwekezaji wa mabilioni ya dola.

Mahitaji ya ndani kutoka viwandani, uzalishaji umeme, mbolea na mauzo yanayotarajiwa kutoka ukanda wote yatakuwa sehemu muhimu ya soko la gesi iliyoko baharini kwa siku zijazo.

Lakini mahitaji ya sasa na miundombinu inayohitajika kupeleka gesi kwa watumiaji wa mwisho, kunahitaji maendeleo makubwa kabla ya kufikia kiwango kinachohitajika kuhalalisha uwekezaji huo mkubwa.

Waziri wa Nishati, Januari Makamba anasema katika kipindi cha miaka 60 katika sekta ya mafuta na ges mafanikio mbalimbali yamepatikana.

Anasema Serikali imetoa Sh. trilioni 57.54 mwaka 2021 kwa ajili ya ugunduzi uliowezesha kuanza kutumika kwa gesi asilia kama chanzo cha nishati, hususan kwa kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na kwenye magari.

Anaongeza kuwa viwanda 52 Jijini Dar es Salaam, mkoani Pwani na Mtwara vinatumia gesi asilia. Aidha, vituo viwili vya kushindilia na kujazia gesi asilia kwenye magari jijini Dar es Salaam na Mtwara vinafanya kazi.

“Asilimia 60 ya umeme unazalishwa kwa kutumia gesi asilia, Sh. trilioni 38 ambazo zingetumika kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya mitambo ya umeme na ya viwandani,” anasema.

Licha ya hivyo serikali imetoa sh bilioni 208 katika Mfuko wa Mafuta na Gesi kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 baada ya kukamilika Ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara/ Songosongo hadi Dar es Salaam.

Anaongeza kuwa mapato ya Sh. bilioni 441 yanayotokana na kodi mbalimbali kuanzia mwaka 2015 baada ya kukamilika kwa mradi wa Bomba la Kusafirisha Gesi Asilia kutoka Mtwara/ Songosongo hadi Dar es Salaam.

Serikali ilipata Sh. bilioni 10 katika mwaka 2018/2019 na mwaka 2019/20 ikiwa ni gawio (Dividend).

Haya hivyo magari 750 yamewekewa mfumo wa matumizi ya nishati ya gesi asilia hayo ni mafanikio makubwa.

“Shilingi bilioni 462 huokolewa kila mwaka ikilinganishwa na kabla ya mfumo husikakuanza kutumika, takribani sh bilioni 391 huokolewa kila mwaka ikilinganishwa demurrage zilizokuwa zikilipwa kabla ya mfumo wa BPS,” anasema.

Anasema kampnuni 1,000 zimeorodheshwa katika kanzidata inayomilikiwa na EWURA ikishirikiana na PURA iliyowezesha kampuni hizo kushiriki katika miradi mbalimbali.

Serikali imewezesha kusainiwa kwa Mkataba kati ya Nchi Hodhi na Wawekezaji (Host Government Agreement – HGA), kusainiwa kwa Mkataba wa Ubia baina ya Wawekezaji (Shareholders’ Agreement – SHA).

Pia kukamilika kwa majadiliano na kuridhiwa kusainiwa kwa Mikataba ya uendeshaji wa Bandari ya Chongoleani na Mikataba ya ukodishaji wa ardhi ya mradi kwa maeneo ya kipaumbele na mkuza wa bomba; Kukamilika kwa malipo ya fidia kwa eneo la Chongoleani itakapojengwa Bandari.

Kuendelea na ulipaji wa fidia kwa Wananchi wanaopisha ujenzi wa mradi; Utoaji wa elimu kwa wananchi katika maeneo yanayopitiwa na mradi ni kazi endelevu; na Kusainiwa kwa mkataba wa nchi zinazotekeleza mradi (Intergovernmental Agreement-IGA).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *