Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
IBARA ya 31(a) ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 inazungumzia kwa msisitizo suala la kuongezeka kwa ajira kutokana na kukua kwa uchumi katika sekta mbalimbali za uzalishaji na utoaji huduma pamoja na kutekeleza mikakati na mipango mbalimbali ikiwemo Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji Nchini.
Aidha, Ibara ya 81 inabainisha kwamba, CCM inatambua kuwa huduma za afya ni muhimu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za maendeleo ya nchi.
Hii ndiyo sababu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiboresha sekta ya afya, ikiwemo kutoa ajira mpya ili kuongeza watumishi pamoja na kutenga fedha nyingi za dawa na vitendanishi.
Na kwa Mwaka wa Fedha 2024/25, tayari Serikali imekwishatangaza ajira mpya 9,483 za watumishi wa sekta hiyo, ambao kimsingi watakwenda kutekeleza vipaumbele 10 muhimu vilivyowekwa mwaka huu katika jitihada za kuboresha sekta ya afya, ambapo kwa mwaka 2024/25 Wizara ya Afya imetengewa Shs. 1,311,837,466,000.00ili kutekeleza malengo na vipaumbele iliyojiwekea, huku Shs. 679,570,246,000.00 kati ya fedha hizo ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Shs. 632,267,220,000.00 kwa matumizi ya kaidwa.
Utekelezaji wa vipaumbele hivyo 10 ni mwendelezo wa jitihada zilizofanywa na Rais Samia katika kuleta mageuzi makubwa kwenye sekta ya afya ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake.
Siyo siri kwamba Rais Samia ameendelea kuipa kipaumbele Sekta hiyo kwa kutoa miongozo, maagizo na maelekezo mbalimbali yaliyolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini.
Vipaumbele vilivyowekwa mwaka huu ujao wa fedha ni; Kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa na kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya Zahanati hadi Taifa.
Vipaumbele vingine ni; Kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini; Kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na watoto wachanga; na Kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika Sekta ya Afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi.
Aidha, vipaumbele vingine ni Kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini; Kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala; na Kuimarisha upatikanaji wa huduma za magonjwa ya kuambukiza, magonjwa yasiyoambukiza na magonjwa ya mlipuko.
Katika hotuba yake, Waziri Ummy alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu; na kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.
Vipaumbele vyote hivyo vimetengewa kiasi cha Shs. 1,311,837,466,000 ambapo serikali itatumia afua (intervention) 89.
Katika kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa, kiasi cha Shs. 117,611,588,304.00 kimetengwa.
Shs. 115,369,238,904.00 kati ya hizo zitatumika kuendelea kuimarisha utekelezaji wa afua za chanjo kwa kuwafikia watoto (surviving infants) 3,117,564 wenye umri chini ya miaka miwili, wasichana 871,429 wenye umri wa miaka tisa na wajawazito 3,298,437.
Serikali imetenga pia Shs. 1,607,700,000.00 kutekeleza afua za lishe ikiwa ni pamoja na kuendelea kuhimiza unyonyeshaji na ulishaji sahihi wa watoto, elimu ya lishe kwa jamii na kuimarisha mpango wa kuongeza virutubishi kwenye vyakula ambapo ununuzi na usimikaji wa mashine 300 za kuongeza virutubishi (Dozifiers) utafanyika.
Si hivyo tu, bali Serikali imetenga pia Shs. 634,649,400.00 kuimarisha utekelezaji wa afua za usafi na afya mazingira katika jamii, mipakani, taasisi za umma na binafsi ikiwemo kutekeleza kampeni ya mtu ni afya awamu ya pili, na imetenga pia Shs. bilioni 1 kuendeleza utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.
Kiasi cha Shs. 219,010,767,716.00 kimetenga katika kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa na vituo vya kutolea huduma za afya katika ngazi zote ili kutekeleza afua tano.
Afua hizo na fedha zilizotengwa zikiwa kwenye mabano ni; Kununua, kutunza na kusambaza dawa na bidhaa nyinginezo katika ngazi zote za utoaji wa huduma za afya (Shs. bilioni 200); kuimarisha upatikanaji wa damu salama (Shs. 3,503,771,816.00); Kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini (Shs. 8,596,534,400.00); Kuimarisha na kuunganisha mifumo ya Tehama katika vituo vya kutolea huduma ili kuboresha ufanisi, kuimarisha udhibiti na kupunguza gharama katika utoaji wa huduma za afya (Shs. bilioni 2); na Kuimarisha ubora wa huduma za Uuguzi na Ukunga katika ngazi zote za kutolea huduma kwa vituo vya umma na binafsi (Shs. 4,910,461,500.00).
Katika kutekeleza kipaumbele cha tatu, jumla ya Shs. bilioni 6 zimetengwa ili kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ambazo zitatekeleza afua tano.
Afua hizo ni; Kufanya mapitio ya mkakati wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia huduma za Afya; Kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote nchini ikiwemo mfumo wa utambuzi wa wanufaika pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya; Kuanza mchakato wa kuanzisha Chombo cha Kitaifa cha Udhibiti wa bei za huduma za afya katika ngazi zote; Kuimarisha uhai na ustahimilivu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya; na Kuimarisha ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Kipaumbele namba nne kimetengewa Shs. 17,189,250,000.00 ili kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Afua zitakazotekelezwa kwenye kipaumbele hiki ni; Kununua na kusambaza dawa muhimu za uzazi salama (Magnesium sulphate, Oxytocin, FeFo na SP) pamoja na dawa za uzazi wa mpango, dawa kinga za minyoo, dawa za kuongeza damu, dawa za Malaria, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; Kuimarisha upatikanaji wa dawa bila malipo kwa ajili ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano ikiwemo dawa za kutibu nimonia na kuharisha; na Kujenga, kukarabati na ununuzi wa vifaa tiba vya wodi 100 maalum za watoto wachanga (Neonatal Care Unit – NCU) wagonjwa na waliozaliwa na uzito pungufu.
Kwenye kipaumbele namba tano, Shs. bilioni 74 zimetengwa ili kuimarisha upatikanaji wa wataalam katika Sekta ya Afya katika fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi ambapo afua tano zitatekelezwa.
Afua hizo na kiasi cha fedha kikiwa kwenye mabano ni; Kuendelea kutoa ufadhili wa mafunzo ndani na nje ya nchi kwa wataalam wa ngazi ya ubingwa na ubingwa bobezi 1,300 (wataalam wapya 600, wataalam wanaoendelea 700) na kufadhili mafunzo ya kada za kati za kimkakati (Shs. bilioni 9); Kutoa mafunzo ya afya ya kada za kati katika vyuo vya afya vya umma (Shs. bilioni 10); Kugharamia mafunzo kwa vitendo ya watarajali wa kada mbalimbali za afya (Shs. bilioni 54); Kujenga na kukarabati miundombinu ya vyuo vya mafunzo ya Afya vya Umma (Shs. bilioni 1); na Kuanzisha kozi mpya ili kukidhi mahitaji ya sasa ya Sekta ya Afya.
Katika kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi nchini, Serikali imetenga kiasi cha Shs. 89,858,609,000.00 kutekeleza afua 10.
Hii ni pamoja na kuendelea kutoa huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi katika Hospitali ya Taifa, Hospitali maalum, Kanda na Mikoa pamoja na kuanzisha huduma mpya kulingana na mahitaji, ikiwemo: Kuanza hatua za awali za kuanzisha huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa kutumia Artificial Intelligence – Robbot katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI); Upandikizaji wa figo Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando; na Upandikizaji wa ujauzito katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa Dodoma.
Afua nyingine ni kuwekeza katika vifaa tiba vitakavyowezesha utoaji wa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi ikiwemo ununuzi wa Mitambo ya kupima na kutibu moyo bila kufungua kifua (Cathlab) mbili kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya na Chato na mtambo kwa ajili ya uchunguzi na Tiba ya Saratani (LINAC) kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando
Ndani ya kipaumbele hiki, Serikali itaendeleza ujenzi wa miundombinu katika Hospitali 6 za Rufaa za Kanda za Chato, Mtwara, Mbeya, KCMC, Bugando, Benjamin Mkapa, ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi Kigoma na Hospitali 28 za rufaa za mikoa; Kuendeleza ujenzi wa kituo cha matibabu ya Saratani tawi la Taasisi ya Saratani Ocean Road – Mbeya; na Kuanzisha tawi la Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Kanda ya Ziwa (JKCI Chato).
Afua nyingine ni kuanza hatua za awali za maandalizi ya Taasisi ya Sayansi ya Tiba ya Magonjwa ya ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu ili kuimarisha huduma za upasuaji wa ubongo na mishipa ya fahamu nchini; kugharamia huduma za matibabu ya ubingwa bobezi ndani ya nchi hususan kupandikiza figo, kupandikiza uloto, kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto na kufanya upasuaji wa ubongo bila kufungua fuvu ili kuwasaidia wananchi wasio na uwezo sambamba na kuwajengea uwezo wataalam wa ndani kutoa huduma hizo kwa umahiri zaidi; na kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Magonjwa ya Damu cha Afrika Mashariki katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Aidha, afua nyingine ni kuimarisha mifumo ya kielektroniki katika Hospitali zilizoteuliwa ili ziweze kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kupitia Tiba Mtandao (Telemedicine) ndani na nje ya nchi; na kuendelea kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi kwa wagonjwa kutoka nje ya nchi (Tiba Utalii).
Katika kuendeleza na kusimamia afua za Tiba Asili na Tiba Mbadala, Serikali imetanga Shs. bilioni 1.5 ili kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Tiba Asili na Tiba Mbadala; kuendeleza huduma za Tiba Asili ikiwemo mashamba ya miti dawa katika mikoa mbalimbali likiwemo shamba la Mzenga B Kisarawe; Kununua ardhi na kufanya usanifu wa ujenzi wa Hospitali maalum ya kitaifa ya kutoa huduma jumuishi za Tiba Asili na Tiba Mbadala; na Kuongeza Hospitali zinazotoa huduma jumuishi za Tiba Asili kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa saba hadi 14.
Kipaumbele namba tisa cha kuimarisha udhibiti wa Magonjwa ya Kuambukiza, Magonjwa Yasiyoambukiza, Magonjwa ya Mlipuko na Huduma za Afya za Dharura kimetengewa Shs. 84,864,241,569.00.
Fedha hizo zitatumika katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria kwa kununua na kusambaza vyandarua vyenye dawa kwa jamii, kununua vitendanishi na dawa ili kuwezesha ugunduzi na matibabu ya ugonjwa wa Malaria; na Utekelezaji wa Mpango wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma kwa kununua vifaa, vifaa tiba, vitendanishi na dawa.
Afua nyingine ni; utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi, Homa ya Ini na magonjwa ya ngono nchini kwa kununua vitendanishi vya kupima magonjwa hayo pamoja na dawa kinga na dawa za kufubaza VVU.
Nyingine ni, kutoa elimu kwa umma kuhusu vichochezi na visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo tabia bwete, uzito uliokithiri, matumizi ya sukari, chumvi, na mafuta kupita kiasi pamoja na kuelimisha kuhusu athari za matumizi ya tumbaku na unywaji wa pombe kupita kiasi; na kuimarisha upatikanaji wa dawa za kutibu magonjwa yasiyoambukiza.
Aidha, afua nyingine ni kutoa mafunzo kwa watoa huduma za magari ya wagonjwa (paramedics) kwa kushirikiana na Vyuo vya kati na Vyuo Vikuu nchini; na kuimarisha Mfumo wa Kitaifa wa Uratibu na Usimamizi wa Afua za Afya ya Jamii ikiwemo kuanzisha Taasisi ya Taifa ya Afya ya Jamii.
Kuhusu kuimarisha huduma za Afya ya Akili, huduma za utengamao na Tiba Shufaa hususan kwa watoto, wazee na wenye ulemavu, Serikali imetenga Shs. 9,318,528,988.00.
Fedha hizo zitasaidia kutoa elimu kwa umma kuhusu vihatarishi vya afya ya akili na namna ya kukabiliana navyo; kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za afya ya akili katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Hospitali za Halmashauri; kuimarisha upatikanaji wa dawa za afya ya akili; na kuanzisha huduma za afya ya akili kwa njia ya mtandao.
Afua nyingine ni kuanzisha huduma tatu za utengamao (Fiziotherapia, Tiba Kazi (occupational therapy), Matamshi na Lugha (Speech and language therapy) katika Hospitali za Rufaa za Mikoa 10; kuimarisha miundombinu ya kutolea huduma za utengamao katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na kuendeleza utoaji wa huduma za utengamao kuanzisha kituo cha umahiri cha huduma za utengamao; ununuzi wa dawa, vifaa na vifaa tiba vya kutolea huduma za utengamao pamoja na vifaa saidizi ikiwemo mikongojo kwa wazee; na kuratibu uanzishwaji wa Klabu za Afya za Wazee katika ngazi ya Halmashauri.
Shs. 3,508,968,000.00 kwa ajili ya kutekeleza kipaumbele cha 10 ambacho ni kusimamia tafiti na matumizi ya matokeo ya tafiti mbalimbali za afya.
Afua zitakazotekelezwa chini ya kipaumbele hiki ni; tafiti za magonjwa yasiyoyakuambukiza ikiwemo Saratani, ufuatiliaji wa usugu wa vimelea dhidi ya dawa, utafiti juu ya changamoto ya Afya ya Akili, utafiti juu ya matumizi ya Energy Drink, utafiti kuhusu Nguvu za Kiume, na utafiti kuhusu dawa za Tiba Asili.