Na Danie Mbega, Dar es Salaam
JUMAPILI, Desemba 31, 2023, wakati akitoa salamu za Mwaka Mpya 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliliagiza Shirika la Reli nchini (TRC) kuhakikisha danadana zinakwisha na safari za treni ya mwendokasi (SGR) zinaanza mara moja.
Na Rais Samia alitoa muda maalum, kwamba mpaka kufikia mwezi Julai 2024, safari hizo kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma ziwe zimeanza.
“Wananchi wamechoshwa na vijisababu, wanataka kuona reli ikifanya kazi. Sasa, naelekeza, ifikapo mwisho wa mwezi Julai 2024, safari kati ya Dar es Salaam hadi Dodoma zianze,” alisema.
Awali ahadi ya kuanza kwa safari hiyo, ilitolewa na Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa, akisema zingeanza Desemba 2022, lakini haikutekelezeka.
Ahadi hizo hazikuishia kwa safari za Dar es Salaam-Dodoma pekee, zilitolewa hata kwa safari za Dar es Salaam-Morogoro bila mafanikio.
Hali hiyo ilisababisha kukosekana kwa matumaini ya utekelezwaji wa ahadi hizo.
Katika kutekeleza agizo hilo la mkuu wa nchi, hatimaye Jumatano, Juni 12, 2024 TRC ikazindua kampeni ya uelewa kuhusu huduma za usafiri wa treni ya SGR ambazo zinaanza rasmi leo hii, Ijumaa, Juni 14, 2024, huku safari za kutoka Dar es Salaam-Dodoma zikitarajiwa kuanza rasmi mwishoni mwa mwezi Julai 2024.
Akasema TRC imeanza na Dar es Salaam-Morogoro kama hatua ya awali zitakazowezesha kupata uzoefu na kutatua changamoto zitakazojitokeza, ili kuboresha safari zitakazoendelea.
“Shirika litaanza kutoa huduma za awali za usafiri wa treni katika Reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro ifikapo Juni 14, 2024, hii ikiwa ni sehemu ya kuendelea kujifunza teknolojia hiyo mpya nchini na kujiridhisha mifumo mbalimbali ya uendeshaji huduma za usafiri wa treni kabla ya kuanza rasmi safari ya kutoka Dar es Salaam – Dodoma ifikapo Juali 25, 2024,” alisema Kadogosa, Mkurugenzi wa TRC.
Kadogosa akawataka wananchi kuendelea kushirikiana kutunza miundombinu ya Reli hiyo kwani ni mali ya Watanzania wote na imejengwa kwa fedha za walipakodi na kuongeza kwamba, kuanza kwa huduma hiyo ya usafiri itasaidia kuongeza Pato la Taifa.
Wanaotarajia kutumia usafiri huo watahakikishiwa ulinzi wa kutosha kuanzia abiria na mizigo kwa ujumla.
“Jambo hili ni muhimu sana ni usalama wa Reli yetu, usalama wa abiria na mizigo, kwani kutakuwa na CCTV Camera, tutakuwa na wataalamu wetu ambao watakuwa wanaangalia kila kinachoendelea kwenye treni yetu kwa saa 24, pia uwepo wa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na askari ndani ya treni ambao watasafiri nasi mwanzo hadi mwisho.
“Kwenye miundombinu, pamoja na kufanya doria, stesheni zetu zote zina vituo vya polisi na tuna imani kuwa kutakuwa na utaratibu wa kuwepo na askari huko njiani, pia askari watafanya doria, tutakuwa na walinzi watakuwa wanafanya kazi saa 24,” akasema Kadogosa.
Nauli za treni
Abiria wanaweza kukata tiketi kwa njia ya mtandao au kupitia madirisha ya kukatia tiketi ndani ya stesheni kwa njia ya mtandao na ili kuepukana na msongamano, abiria atatakiwa kukata tiketi wiki moja au siku 3 kabla ya safari.
Tayari Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) wameshatangaza nauli na hivyo wateja wawe tayari kwa safari na gharama iliyowekwa ni rafiki na mtu yeyote atamudu.
“LATRA wametangaza nauli za daraja la kawaida, lakini tutakuwa na treni za aina tatu, treni ya kawaida itakayosimama kila sehemu, tutakuwa na treni za moja kwa moja (Express) na treni mchongoko,” akasema Kadogosa.
Kwa mujibu wa Latra, nauli za safari ya treni hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro kwa watu wazima na watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 12 ni Shs. 13,000 huku watoto wa chini ya miaka minne watalipa Shs. 6,500 kwa daraja la kawaida.
Ofisa Biashara wa TRC, Lilian Mselle amesema njia mbalimbali zitatumiwa na abiria kununua tiketi ikiwemo GePG (Control Number), Visa au Master card na kupitia mitandao mbalimbali ya simu.
“Hatua hii inalenga kupunguza malipo ya fedha ya mkono kwa mkono na kuhamasisha malipo kwa njia ya mtandao. Chakula kitauzwa kwenye vituo kwa bei nafuu kwa, sababu hiyo hakuna abiria atakayeruhusiwa kuingia kwenye treni na chakula,” amesema.
Watakaoruhusiwa kuingia na vyakula ni wanawake wanaonyonyesha na vyakula hivyo vinapaswa kuwa vya watoto wenye umri wa kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja.
Amesema katika daraja la biashara, abiria ataruhusiwa kubeba mzigo wa kilo 20 bure.
Kulingana na LATRA, nauli za treni hiyo kutoka Dar es Salaam-Dodoma, kwa daraja la uchumi ni Shs. 70,000, biashara Shs. 100,000 na daraja la kibiashara la kifalme ni Shs. 120,000.
Mbali na Dodoma, Latra ilizitaja bei hizo ambapo anayekwenda Pugu atalipa Shs. 1,000, Soga Shs. 4,000, Ruvu Shs. 5,000, Ngerengere Shs. 9,000, Morogoro Shs. 13,000, Mkata Shs. 16,000, Kilosa Shs. 18,000, Kidete Shs. 22,000, Gulwe Shs. 25,000, Igandu Shs. 27,000, Dodoma Shs. 31,000, Bahi Shs. 35,000 na Makutupora Shs. 37,000.
“Kulingana na mahitaji ya soko la wateja, TRC imepanga kuanza na treni mbili kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na Dodoma hadi Dar es Salaam kila siku,” akasema Kadogosa.
Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara (TCB), Adam Mihayo, anasema katika safari hizo za Reli ya SGR, TCB wameshirikiana na TRC katika kukusanya mapato katika vituo vya kukatia tiketi.
Lakini akasema, TCB wameshirikiana na TRC kufanikisha kuleta vichwa vya treni na mabehewa kutoka Ujerumani.
“Ushirikiano wetu na Reli ya Tanzania unaakisi dhamira yetu ya pamoja ya kuelewa mahitaji ya watanzania na kuchangia katika ukuaji wa amaendeleo ya kiuchumi na mafanikio ya Taifa letu.
“TCB tutaendelea kushirikiana na shirika la Reli Tanzania ili kuhakikisha matarajio ya Mhe. Rais katika mradi huu yanaweza kutimia,” akasisitiza Mihayo.
Mkuu wa Mradi wa Yapi Merkezi, Mehmet Firat, akasema kuanza kwa safari hizo ni historia, kwani ni mradi walioanza kujengwa tangu awali.
“Tumejenga SGR kutoka Dar es Salaam-Morogoro na kila kitu kimekamilika, tunatarajia itatumika kukuza uchumi wa nchi,” akasema.
Kwa mujibu wa Mehmet, Tanzania imejenga SRG bora zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa ni hatua kubwa kwa wananchi wake na sekta binafsi kuitumia.
Wananchi wengi wamefurahishwa nah atua ya kuanza kwa usafiri wa treni hizo, wakisema itarahisisha usafiri kwa kiwango kikubwa.
Juma Sekwao, ameitaka TRC kusimamia kikamilifu ratiba watakazokuwa wanazipanga ili kuepuka kukosa watu na kuepusha usumbufu kwa abiria.
“Kuna saa za watu wa Afrika, saa 2:00 asubuhi unaambiwa ndiyo mnaondoka mnaondoka saa 3 asubuhi, au mnaambiwa saa 11 asubuhi mnaondoka saa 1 asubuhi, hii huwa inakera ndiyo maana watu huwa wanaangalia wapi kuna unafuu unaoendana na ratiba zao walizopanga,” akasema Sekwao.
Umeme wa uhakika
Licha ya kwamba kumekuwepo na kukatika kwa umeme mara kwa mara, lakini Kadogosa amewatoa hofu wananchi kwamba hakutakuwa na changamoto yoyote kwa vile treni hiyo itakuwa na njia yake maalumu ya kusafirishia umeme, hivyo kutoathirika na kukatika kwa umeme kunakoendelea.
Kadogosa alisema TRC haina tatizo wala hofu kwa kuwa wanayo njia maalumu ya usafirishaji umeme kwa ajili ya treni ambayo haifungamani na njia yoyote.
Alisema hiyo inawafanya kuwa na uhakika wa nishati na njia pekee inayoweza kufanya wakose umeme wa kuendeshea treni ni pale nchi nzima itakapokuwa gizani.
“Hata hivyo, sisi si watumiaji wakubwa wa umeme, watu wanadhani labda treni itatumia megawati 2,000, hapana, tuna imani kuwa umeme unaozalishwa na Tanesco na wanaotarajia kuingiza katika gridi utatosheleza sisi kuendesha treni,” alisema Kadogosa.
Alisema ikiwa umeme utakosekana nchi nzima na treni kushindwa kufanya kazi, katika maeneo yao ya maunganisho ya treni (shunting) kuna vichwa vya treni vinavyotumia dizeli ambavyo vinaweza kutumika kama mbadala.
“Baadaye tutakuwa na ‘hybrid’ ambazo tutaagiza hizi zitakuwa zikitumia umeme ikitokea dharura unaweza kubadili na kutumia mafuta,” alisema Kadogosa.
Alisema vichwa vya treni vya ‘hybrid’ pia vipo vya aina tofauti ikiwemo vilivyowekwa betri ambayo ina uwezo wa kujichaji kadri treni inavyofanya kazi na baadaye nishati hiyo inaweza kutumika kwa dharura pindi kunapokuwa na tatizo.
Na mnamo Machi 27, 2024, Meneja Maendeleo na Biashara wa Tanesco, Mhandisi Magoti Mtani, alisema reli ya SGR itakuwa na njia (lots) tatu za kusafirishia umeme wa uhakika muda wote ili kuifanya treni hiyo itoe huduma kwa uhakika.
“Umeme wake utatoka katika njia ambazo zimeunganishwa kutoka maeneo mbalimbali na hili limeweza kufanyika kwa Lots 3 na ya kwanza ni Msamvu – Ihumwa (Lot 1 ina double circuits ambapo inajumuisha Lot 1 – 2 kwa pamoja na Lot ya 3 ni kutoka Isaka – Mwanza,” alisema.
Wamiliki wa mabasi wanena
Kutangazwa kwa nauli rafiki na kuanza kwa safari za treni ya SGR kumewaibua wamiliki wa mabasi nchini, ambao wanasema nauli hizo ni shindani, ingawa ubora wa huduma ndio utakaopimwa na wasafiri.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), John Priscus, amekaririwa akisema nauli zilizotajwa ni shindani lakini ubora wa huduma ndiyo utakaomfanya mwananchi kuchagua aina ya usafiri anaotaka kutumia.
“Haiwezi kutuondoa sisi bado kuna vitu mteja anavihitaji, kila mtu ana njia yake, sehemu anayoshukia mtu, urahisi wa upatikanaji wa huduma husika, hivyo si rahisi kuua biashara yetu,” akasema Priscus.
Akatolea mfano wa uwepo wa baadhi ya nchi ambazo zina mtandao wa reli karibu kila eneo lakini bado kuna mabasi yanayotoa huduma kwa wananchi wake kutokana na treni kushindwa kufika sehemu hizo.