KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema mazungumzo baina ya serikali kuhusu mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi asilia (LNG) yamefikia mwishoni na kwamba manufaa yanayotarajiwa ni kuweza kuanza kunufaika na gesi ambayo imegunduliwa kwa muda mrefu na haijaweza kutumika kwa kiasi kikubwa.
Aidha Mramba amesema kuwa asilimia 64 ya umeme wote unaotumika nchini unazalishwa kwa kutumia gesi asilia na kwamba manufaa ya gesi hiyo ni zaidi ya kuzalishia umeme.
Mhandisi Mramba aliyabainisha hayo jana alipotembelea banda la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema mradi wa LNG ndio utakaowezsha gesi ya Tanzania kuuzwa nje ya nchi na kwamba zipo namna chache ya kutekeleza jambo ikiwemo ya kutengeneza mabomba na kuisafirisha kwa njia hiyo kwenda nchi za karibu.
“Serikali imetekeleza hilo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na sasa tuko katika hatua za ndani ili kukamilisha mchakato huo, pia tunapokuwa na miradi mikubwa kama hii tunasababu ya kujiandaa ili tuweze kunufaika zaidi,” amesema Mramba.
Amefafanua kuwa, tangu gesi katika mradi huo igunduliwe ilitumika katika kuzalisha umeme tu, na kwamba zaidi ya asilimia 64 ya nishati hiyo inayotumika nchini inazalishwa na gesi asilia.
“Manufaa ya gesi ni zaidi ya kuzalishia umeme kwasababu mradi wa LNG utawezesha kuuza malighafi hiyo kwenye masoko ya kimataifa na hiyo itawezesha kuiletea Tanzania fedha za kigeni na kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye uchumi wa nchi yetu,”
Ameongeza kuwa mradi huo utaongeza ajira pamoja na matumizi mengine ya gesi katika viwanda na huduma mbalimbali ambazo zitakuwazikitolewa na watu watakaokuwa wakifanya kazi katika mradi.
Vilevile, amesema kwa sasa wanajiandaa ili mapema 2024 waanze kutangaza tena kutoa vitalu kwa wawekezaji mbalimbali wanaofanya tafiti ya kugungua gesi au mafuta na kwamba jambo hilo liko katika hatua za maandalizi.
“Mkakati wa serikali katika matumizi ya nishati nchini ni kuwa na mchanganiko wa nishati za aina mbalimbali ambao utahakikisha usama wa nishati muda wote, na sasakwa kiasi kikubwa uzalishaji wa umeme unategemea gesi asilia, ikifuatiwa na maji na kiasi kidogo cha vyanzo vingine,” amesema Mramba.
Hata hivyo, amesema wanapoelekea mchango wa nishati jadidifu (kuzalisha umeme kwa kutumia joto ardhi, sola, upepo na Haidrojen), utaongezeka na kwamba ni vyanzo vitakavyotazamwa zaidi.
Amebainisha kuwa utafiti uliofanyika umeonyesha kuwa Tanzania inauwezo mkubwa wa kuzalisha umeme wa jua na upepo, na kwamba taratibu za kuanza kuupata umeme huo zimeanza na makontrakta wako saiti huko Kishapu.
Pia amesema huduma zinazotolewa na TANESCO zimeendelea kuboreshwa, na kwamba mtu akiomba umeme anapata kwa wakati na malalamiko yanazidi kupungua akieleza kuwa wizara itaendelea kushirikia na shirika hilo kuhakikisha wanaboresha huduma zao zaidi.