CHUO Kikuu Dodoma (UDOM), kimebuni mfumo madhubuti unaodhibiti hali ya hewa, ikiwemo unyevunyevu na joto, kwenye kilimo cha kwenye ‘greenhouse’.
Akizungumza na Tanzania Leo, katika maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Mwanataaluma kutoka Idara ya Fizikia, Ndaki ya Sayansi Asilia na Hisabati, UDOM, Paschal Magambo, amesema lengo la kubuni mfumo huo ni kumrahisishia mkulima kubaini kulima zao la aina gani, kulingana na mazingira ya eneo au Mkoa husika.
Amefafanua kuwa kabla ya ubunifu huo walifanya utafiti na kubaini zilizopo hazina uwezo wa kudhibiti hali ya hewa kulingana na eneo husika.
“Greenhouse’ tuliyobuni ni tofauti na zilizopo sokoni na zinazotumiwa kwenye kilimo nchini. Kwa mfano ‘greenhouse’ ya hapa Dar es Salaam, na iliyopo Mafinga au Makete kwenye baridi, zikifanana, si sawa.
Ameongeza kuwa kufanana kwa ‘greenhouse’ wakati mazingira ni tofauti ya joto na baridi, kunamfanya mkulima asibaini ni zao gani linafaa eneo hilo.
“Kwahiyo nikaona nije na huu mfumo wa ‘greenhouse control system’ ambao unaweza kuchagua aina ya zao, mfano tikiti au nyanya na itakuonyesha ni joto la aina gani linahitajika, ili zao likue.
“Hata hivyo ubunifu huu umefanyiwa majaribio na kubaini mfumo huo unaweza kujibadilisha kulingana na mazingira ya sehemu mbalimbali, kwa kutumia kifaa maalumu kitakachofungwa kwenye ‘greenhouse’ na kwamba tofauti na zilizopo sokoni hivi sasa, zimetengenezwa kudhibiti wadudu pekee.
Amebainisha kuwa ubunifu huo ni rahisi kutumiwa na mkulima mwenye elimu ya kiwango chochote, kwa kuwa mfumo unajidhibiti na kwamba kifaa kinachotumika kupima hali hewa hutumia nishati ya umeme au ya jua.
“Ubunifu huu ukiingia sokoni utatatua changamoto kwenye kilimo cha greenhouse. Zao lolote likiwa katika hali ya joto litakuwa na afya kuliko ambalo kutwa lipo kwenye baridi, au zao linalopata jua, joto kwa kiwango kidogo ukuaji wake ni duni. Mfumo huu unaweza kuongeza kiwango cha joto kwa kilimo kinachofanyika maeneo yenye baridi, ili zao lishamiri,” amesema na kuongeza kuwa:
“Ugunduzi huu wa UDOM ambao haujabuniwa tu na mimi peke yangu tumeshirikiana na wenzangu wa chuo, bado haujaingia sokoni, kulingana na njia iliyotumika kutatua tatizo husika kwenye sekta ya kilimo,” amesema Magambo.
Aidha, Mkufunzi kutoka chuo hicho, Dk. Mhandisi, Ombeni Mdee, amesema UDOM imeendelea na ubunifu katika maeneo tofauti huku kikibuni pampu ya maji inayotumia umeme mdogo, ili kupunguza matumizi ya nishati hiyo.